KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AKIPONGEZA KIKUNDI CHA BODABODA RORYA
Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Maalum Lt. Josephine Paul Mwambashi amekipongeza kikundi cha bodaboda cha vijana kutokana na uaminifu wao katika kurudisha mkopo waliopewa na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Bibi Mwambashi ametoa pongezi hizo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Kikundi hicho na kuelezea kufurahishwa kwake kwa namna vijana hao walivyojenga uaminifu na sasa kwa kutumia uaminifu huo wamekopeshwa tena.
“Nataka niwapongeze kwa uaminifu wenu mlioufanya katika biashara zenu na kufanikiwa kurejesha mkopo wa halmashauri kwa wakati na hivyo mkafanikiwa kupata mkopo mwingine tena” alisema Mwambashi.
Hata hivyo aliwataka vijana hao kuzingatia sheria za barabarani wakati wakiendesha pikipiki hizo kwa usalama wa maisha yao na wananchi wengine.
“Kumekuwa na ajari nyingi za pikipiki na kuhatarisha maisha ya madereva, watumiaji wa pikipiki na wakati mwingine hata watumiaji wengine wa barabara kutokana na kutokuzingatia sheria za usalama wa barabarani” alisema Mwambashi.
Hata hivyo Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Rorya kuhifadhi pikipiki moja mpaka wanaopatiwa mafunzo wafuzu na waje na lesseni ya udereva.
Awali akisoma taarifa ya kikundi hicho Mwenyekiti wa Kikundi hicho Bwana James Msigwa ameeleza kuwa kikundi hicho kilipewa mkopo na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya wa shilingi milioni tano ambazo walitumia kununua pikipiki mbili na kuanzisha biashara yao.
“Ule mkopo tulipomaliza kuurejesha ndani ya muda tuliyokuwa tumepangiwa, tukapatiwa tena mkopo mwingine wa kununua pikipiki nyingine mbili ili kupanua mradi wetu.
Bwana Msigwa amesema kuwa kikundi hicho ni cha vijana kumi ambao waliamua kujiunga pamoja na kuanzisha biashara yao.
Kati ya vijana hao vijana watatu wanaleseni za udereva, kijana mmoja analeseni iliyoisha muda wake wa matumizi na vijana wengine sita wapo katika mafunzo ya udereva.
Wakati huo huo Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa amelipongeza Jeshi la Polisi kwa jitihada kubwa linafanya katika kukamata madawa ya kulevya.
Hata hivyo amekataa kuteketeza bangi zilizokamatwa katika Wilaya ya Rorya kutokana na eneo hilo kuwa karibu na makazi ya watu.
Mwenge wa Uhuru leo umeendelea na mbio zake katika Wilaya ya Rorya ambapo umepokelewa katika eneo la Nyanchabakenye kutoka Wilaya ya Tarime na unatarajiwa kukabidhiwa kesho kwa Wilaya ya Musoma katika viwanja vya Mukendo vilivyopo katika Manispaa ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa