Kikao kazi cha Wakuu wa Mikoa saba inayolima pamba hapa nchini pamoja na Wakuu wa Wilaya, Wabunge, viongozi wa vyama vikuu vya ushirika na wadau wa pamba nchini kimefanyika leo katika ukumbi wa uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee ameeleza kikao hicho ni muhimu sana kwa maendeleo ya kilimo cha zao la pamba hapa nchini.
“Ndugu viongozi, elimu tutakayoipata leo tukaitumie katika kuhamasisha kilimo cha pamba na kusaidia kusimamia mfumo mzima wa zao la pamba ili kuinua hali za wakulima wa pamba hapa nchini” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amesema kuwa Mkoa wa Mara unavyama vya ushirika vya msingi 235 ambavyo vinajishughulisha na ukusanyaji na uuzaji wa pamba na vyama vikuu vya ushirika viwili ambapo kimoja kinaratibu biashara ya pamba.
Akizungumzia uzalishaji wa pamba katika Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa Mwaka 2022/2023 Mkoa ulizalisha kilo 6,458,000 za pamba zenye thamani ya shilingi 9,687,000,000 na msimu ujao wa mwaka 2023/2024 Mkoa wa Mara unalenga kuzalisha kilo 7,079,825 za pamba.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidigitali kwenye shughuli za kilimo unaenda kuongeza usimamizi, ufanisi na upatikanaji wa takwimu sahihi kwa ajili ya mipango na bajeti ya uendelezaji wa sekta ya kilimo.
Mkuu wa Mkoa ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika na taasisi zote zilizoratibu kikao kazi hicho kwa kufikiria usimamizi wa mavuno yap amba wakati huu kukiwa na muda bado wa kuendelea kutoa elimu kwa wakulima na viongozi wa vyama vya ushirika kuhusu mifumo inayopendekezwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania Bwana Marco Charles Mtunga ameeleza kuwa mfumo wa kidigitali wa usimamizi wa mauzo ya pamba utasaidia sana katika mambo mengine ambapo utawezesha usajiri wa wakulima, kuimarisha mifumo ya kugawa pembejeo kwa wakulima na kadhalika.
“Kwa hali ilivyo sasa ugawaji wa pembejeo za kilimo unakuwa na wizi ndani yake kwa kuwa wakulima hawajulikani walipo, wanalima kiasi gani na mahitaji yao ni nini, lakini mfumo huu utatoa suluhisho la changamoto hizo”. Alisema Bwana Mtunga.
Aidha, Bwana Mtunga amezungumzia umuhimu wa kujenga uwazi katika mfumo mzima wa kilimo na biashara ya pamba hapa nchini ili kuhakikisha wakulima wanapata tija na wahusika wengine wote wanufaike kulingana na stahili zao.
Bwana Mtunga ameeleza kuwa mfumo wa ununuzi wa mazao utasaidia pia kuonyesha kiasi gani cha mazao yaliyopatikana, wanunuzi wa mazao hayo, kiasi gani cha mazao ambayo bado hayajanunuliwa na bei ya mazao iliyofikiwa katika mnada.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mheshimiwa Dkt. Yahya Nawanda na wakuu wa Wilaya waliowawakilisha wakuu wa Mkoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Stakbadhi za Ghala, taasisi za kifedha, simu za mkononi na wadau wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa