Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amefanya ziara katika Wilaya ya Butiama ambapo ametembelea makazi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika eneo la Mwitongo, Butiama.
Akiwa nyumbani kwa Baba wa Taifa, amepokelewa na wanafamilia wakiongozwa na mtoto wa Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere na kufanya mazungumzo na wanafamilia na kutembelea kaburi la Baba wa Taifa.
Katika eneo hilo pia, Mkuu wa Mkoa amezungumza na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama na kuitaka kubadilisha mbinu za kushughulikia uhalifu badala ya kufuatilia uhalifu ukiwa umefanyika , wafuatilie wahalifu wakiwa kwenye mipango ya uhalifu.
“Kazi zenu zikiongozwa na intelijensia, mnaweza kupata taarifa za uhalifu kabla ya uhalifu haujafanyika na kusaidia kuzuia matukio ya uhalifu kabla hayajatokea, hili linawezekana mlifanyie kazi” amesema Mhe. Kanali Mtambi.
Kanali Mtambi amelitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara kushirikiana vizuri na wananchi na kuimarisha polisi jamii katika maeneo mbalimbali ili kuweza kupunguza vitendo vya uhalifu katika jamii na kuwalinda wananchi na mali zao.
Mhe. Mtambi ameeleza kuwa atafanya ziara ya kuzitembelea Wilaya zote za Mkoa wa Mara hivi karibuni kwa ajili ya kujitambulisha na kuahidi atakuwa anaenda Butiama mara kwa mara na hususan nyumbani kwa Baba wa Taifa.
Wakati huo huo, Mhe. Kanali Mtambi amemtembelea Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali David Msuguri na kuzungumza nae nyumbani kwake katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Butiama.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mtambi ameambata na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Kamati ya Usalama ya Wilaya, Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na watumishi wengine.
Hii ni mara ya kwanza kwa Mhe. Kanali Mtambi kutembelea Wilaya ya Butiama baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara tarehe 31 Machi, 2024.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa