Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 29 Mei, 2024 amefanya ziara yake ya kikazi ya kwanza katika Wilaya ya Butiama na kuwataka wataalamu kuifanya Wilaya ya Butiama kuwa kitovu cha biashara mbalimbali katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi amesema hayo alipokuwa anazungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na wananchi wa Butiama katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Butiama na kuwataka wataalamu kuwaongoza wananchi kuchangamkia fursa za kibiashara zilizopo katika Wilaya ya Butiama.
“Wilaya hii inazo fursa nyingi sana za kibiashara ambazo bado wananchi hawajazichangamkia kwa sababu wataalamu hamjawaelimisha kuhusiana na fursa za uwekezaji unaohitajika kwa sasa katika Wilaya ya Butiama” amesema Mhe. Mtambi na kuwataka wataalamu kuwasaidia wananchi kuanzisha na kuendeleza biashara zao.
Mhe. Mtambi amesema kwa sasa Wilaya hiyo ina utulivu na Serikali imeleta fursa kubwa baada ya kuanza ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia, Butiama wenye gharama ya shilingi bilioni 102 katika eneo hilo ambapo ujenzi ukikamilika unatakiwa kuchukua wanafunzi wengi.
Aidha, Mhe. Mtambi ameitaka Wilaya ya Butiama kulitumia vizuri eneo la Makutano kwa ajili ya uwekezaji na biashara kubwa za kuweza kuwakutanisha wananchi wote wa Mkoa wa Mara kukutana hapo na kuuchangamsha Mkoa kiuchumi.
Mhe. Mtambi ameagiza Wilaya ya Butiama kuanzisha Nyama Choma Festival katika mnada wa Kiabakari ambao unafanyika tarehe 06 na 23 ya kila mwezi ambapo wachoma nyama maarufu watashindana kumpata mshindi wa Mkoa ambaye atapewa zawadi.
Aidha, Mhe. Mtambi ameagiza kuanza kwa mbio za maboti katika ambazo atazizindua tarehe 31 Agosti, 2024 na kuwataka viongozi na watendaji wa Wilaya hiyo kuyaandaa vizuri nay eye atashiri katika mashindano hayo.
Kanali Mtambi amesema anatamani kuona Mkoa wa Mara ambapo watu wanapata sehemu nzuri za starehe na shughuli za kuwavutia watalii kutembelea fukwe za Ziwa Victoria jambo ambalo amesema litasaidia kuchochea uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Mara watakaochangamkia fursa hizo.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi wa Wilaya ya Butiama kutumia vizuri jina la Butiama kutokana na historia ya eneo hilo kitaifa na kimataifa kujiletea maendeleo na kuipongeza Wilaya ya Butiama kwa utulivu wa wananchi wake na kuwataka kutumia utulivu huo huo na fursa zilizopo kufanya biashara saa 24 katika Kijiji cha Butiama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Mhe. Peter Wanzagi amemkaribisha Mkuu wa Mkoa katika halmashauri ya Butiama na kueleza kuwa watumishi hawa ndio wanasimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya Halmashauri hiyo.
Mhe. Wanzagi ameeleza kuwa watumishi hao wameiwezesha Halmashauri hiyo kufanya vizuri na kuiwezesha kupata hati safi za ukaguzi kwa miaka mitatu mfululizo.
Bwana Wanzagi amemuomba Mkuu wa Mkoa kusimamia mgawango wa mali za iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambayo iligawanywa mwaka 2012 ambapo mpaka sasa bado hawajagawana mpaka sasa.
Tayari kitabu cha mgawanyo kipo tayari na baadhi ya vikao vimeanza kukaa lakini Halmashauri ya Wilaya ya Musoma haitaki kugawana nao mali zote wamezihodhi na kuomba Mkuu wa Mkoa wa Mkoa apitie nyaraka za mali na madeni yao na kukaa na halmashauri hizo kuhusu mgawanyo huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Christopher Marwa Sigi amemkaribisha Mkuu wa Mkoa katika Wilaya ya Butiama na chama kwa Wilaya kinafanya vizuri kutokana na watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao.
Mhe. Sigi ameeleza kuwa maendeleo ya Wilaya ya Butiama yanatokana na Chama na watumishi kuzungumza lugha moja katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa ameambata na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Butiama, Kamati ya Usalama Wilaya ya Butiama, Mwenyekiti na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama baadhi ya maofisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na watumishi wa Halmashauri ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa