Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amewasili Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara tayari kwa kuanza kutekeleza majukumu yake na kupokelewa na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Menejimenti na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Baada ya mapokezi hayo, Mhe. Mtambi ametembelea Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kwa ajili ya kusaini kitabu cha wageni na kujitambulisha ambapo alipokelewa na Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya siasa Mkoa wa Mara, viongozi na watumishi mbalimbali wa CCM.
Akizungumza na viongozi wa CCM Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Mtambi amewaomba viongozi wa CCM kutoa ushirikiano ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa wa Mara na kuahidi kuwa yeye pamoja na viongozi wengine wa Serikali watatoa ushirikiano kwa CCM Mkoa wa Mara na ofisi yake muda wote ipo wazi kwa ajili ya jambo lolote lenye manufaa kwa Mkoa wa Mara.
Aidha, amesema kuwa amekuja kufanyakazi na atahakikisha kazi inafanyika kwa mchakamchaka ili kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Mara wanapata maendeleo wanayotarajia kutoka kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
“Huko kwenye kazi mkiona cheche zinatokea mjue tupo kazini tunatekeleza majukumu yetu tuliyotumwa kuyafanya, hatutamuonea mtu lakini tutapambana na watu wote wsiofuata taratibu na sheria za Serikali” amesema Kanali Mtambi.
Amevitaja vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na elimu, afya, kutatua migogoro ya ardhi, usalama wa Mkoa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uchaguzi Chama na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 unaendeshwa kwa amani na utulivu katika Mkoa wa Mara.
Kanali Mtambi amekishauri chama kuimarisha mfumo wa kuwa na balozi wa nyumba kumi ili kuweza kuwapata viongozi wa chama kuanzia ngazi ya chini watakaowatumikia wananchi wa Mkoa wa Mara na kutambua matatizo yao.
Mhe. Mtambi pia ametembelea mradi wa ujenzi wa ukumbi wa CCM Mkoa wa Mara unaojengwa kutokana na michango ya wanachama na kupokea taarifa ya ujenzi na hatua ulipofikia mradi huo na kuahidi kuchangia katika ujenzi huo.
Mhe. Mtambi pia ametumia fursa hiyo kuwakaribisha viongozi wa CCM Mkoa wa Mara kwenye makabidhiano ya Ofisi baina yake na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mohamed Mtanda ambayo yanatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa uwekezaji leo mchana.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Mara Bwana Ibrahim Mjanakheri Ibrahim amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kutembelea Ofisi za CCM na kumpongeza kwa kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Bwana Ibrahim ameipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na hususan Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa Chama cha Mapinduzi katika ngazi za Mkoa na Wilaya.
Bwana Ibrahim ameeleza kuwa CCM katika Mkoa wa Mara kina Wilaya za kichama saba, majimbo ya uchaguzi 10, tarafa 20, kata 180, vijiji 487, matawi 803 na mashina 11,689 na CCM imefanya vizuri sana katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika hivi karibuni.
“Katika Kata za Busegwe (Wilaya ya Butiama) na Mshikamano (Manispaa ya Musoma) CCM imeshinda hata baada ya vyama vya upinzani kuungana na kumuunga mkono mgombea mmoja, bado CCM ikashinda, ushindi huu unatoa matumaini kwa chaguzi zinazokuja” amesema Bwana Ibrahim.
Bwana Ibrahim pia ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Mara kwa kukishirikisha chama katika shughuli mbalimbali za Mkoa na taarifa zote muhimu za Mkoa zinatolewa kwa viongozi wa Chama mara kwa mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa