Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amekabidhi ofisi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi katika hafla fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kanali Mtambi amewataka viongozi na watumishi wa umma wa Mkoa wa Mara kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za uongozi na utumishi wa umma na kuweka kipaumbele katika kuwahudumia wananchi.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa tunatimiza wajibu wetu wa kuwatumikia wananchi na kutatua changamoto zao kwa nafasi zetu tulizonazo, sitavumilia uzembe wa aina yoyote na kutoka kwa mtu yoyote” amesema Mhe. Kanali Mtambi.
Aidha, amezitaka taasisi zinazotakiwa kutoa huduma saa 24 kwa siku kuhakikisha zinatoa huduma kikamilifu muda wote ikiwemo hospitali, jeshi na polisi kuhakikisha wanaboresha pia huduma zinazotolewa usiku na siku za mwishoni mwa wiki.
“Kuna hii tabia ukienda hospitali usiku au siku za mwisho wa wiki unaambiwa huwezi kupata vipimo au mtaalamu Fulani hayupo mgonjwa anaambiwa njoo siku nyingine, hili halikubaliki Mkoa wa Mara” amesema Mhe. Mtambi.
Amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kufuata sheria, taratibu na kanuni katika kutekeleza miradi ya maendeleo ili iweze itekelezwe kwa ubora na ikamilike kwa wakati unaotegemewa ili wananchi wapate huduma katika miradi hiyo.
Mhe. Mtambi amesema anataka kupunguza uhalifu katika Mkoa wa Mara na kumtaka Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara kuwashughulikia wahalifu kabla hawajafanya uhalifu na kumtaka kufufua mifumo ya kiintelijensia ifanye kazi ya kubaini uhalifu kabla haujatokea.
Amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Musoma kuhakikisha mlipuko wa kuharisha na kutapika ulioanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma unadhibitiwa na hauenei katika Mkoa wa Mara na kufanya ukaguzi wa usafi wa mazingira mara kwa mara.
Amewaagiza mameneja wa Mkoa wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha kuwa barabara na madaraja yote yanapitika muda wote pamoja na mvua zinazoendelea kunyesha.
Amezitaka Mamlaka na wakala za Maji katika Mkoa wa Mara kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa wananchi na miradi ya maji inakamilika kwa wakati na kutoa huduma kwa wananchi ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mohamed Mtamba amewashukuru viongozi, watumishi na wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ushirikiano mkubwa waliompatia wakati wote akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine yanayosikika kuhusu Mkoa wa Mara kwa watanzania wengine, wananchi wa Mkoa wa Mara ni watu wema, wakarimu na wanapenda maendeleo yao.
Mhe. Mtanda amempongeza Mhe. Mtambi kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuuongoza Mkoa wa Mara na kuwataka watu wa Mkoa wa Mara kumpa ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Hafla ya makabidhiano imehudhuriwa na viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Meya wa Manispaa ya Musoma, Wakuu wa Sehemu na Vitengo vya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, wakuu wa taasisi za umma, wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa