Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo imekagua miradi ya itakayotembelewa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 katika Wilaya za Butiama na Bunda.
Katika Wilaya ya Butiama, Kamati imepokea taarifa za miradi itakayotembelewa na Mwenge katika Wilaya ya Butiama ikiwa ni pamoja na maandalizi ya kumbukizi ya miaka 60 ya Mwenge wa Mwitongo itakayofanyika nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kijiji cha Butiama.
Aidha, Kamati imetembelea mradi wa Zahanati ya Kijiji cha Nyalukolu, mradi wa shamba la miti lililopo katika eneo la zahanati hiyo pamoja na hoteli ya Nabaki Africa inayomilikiwa na Bwana Nyihita Wilson Nyihita iliyopo katika kijiji cha Nyabange.
Baada ya hapo Kamati imepokea taarifa na kukagua miradi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ya Mji wa Bunda na baadaye kutoa maelekezo ya jumla kuhusiana na miradi hiyo.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Kamati imetembelea na kukagua mradi wa Maji wa Sanzate unaotekelezwa na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) na mradi wa barabara ya Karoleni –Nyamzabe unaotekelezwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
Katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, Kamati imetembelea mradi wa Zahanati ya Ligamba B na mradi wa maji machafu unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWASA) na baadaye kufanya kikao cha majumuisho ya miradi ya Halmashauri zote mbili.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Kamati ya Wataalamu na Kamati ya Usalama ya Mkoa na kuhakikisha kunakuwa na hamasa ya kutosha wakati wa mbio za mwenge wa uhuru katika maeneo yao.
Katika ziara hiyo Kamati ya Usalama ya Mkoa imeambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya za Butiama na Bunda, Maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri za Wilaya ya Butiama, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kupokelewa Mkoa wa Mara tarehe 26 Julai, 2024 na kukimbizwa katika Wilaya sita na Halmashauri tisa kabla ya kukabidhiwa Mkoa wa Simiyu tarehe 4 Agosti, 2024.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa