Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 15 Julai, 2024 imefanya ziara katika Wilaya ya Rorya kukagua miradi itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2024.
Ikiwa katika Wilaya ya Rorya, kamati imetembelea mradi wa maji unaotekelezwa na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) kwa kushirikiana na Maji Safi Group katika Kitongoji cha Sokolabolo, Kijiji cha Bukama Wilaya ya Rorya.
Aidha, Kamati imetembelea mradi wa ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa na vyoo 10 katika Shule ya Sekondari ya Bukama na ikiwa hapo, Kamati ilipata fursa ya kusikiliza nyimbo zenye ujumbe wa Mwenge wa Uhuru zilizoandaliwa na wanafunzi wa klabu ya Wapinga Rushwa katika shule hiyo.
Mradi mwingine ni mradi wa ujenzi wa vyoo katika Shule ya Msingi Ngasaro na Daraja la mto Ngasaro linalojengwa na Wakala wa Barabara za mijini na Vijijini (TARURA) na kutembelea mradi wa ukarabati wa Bohari ya Dawa katika Hospitali ya Teule ya Wilaya ya Rorya, Shirati inayomilikiwa na taasisi ya kidini kwa ubia na Serikali.
Kamati iliitaka Halmashauri kutekeleza maagizo yote ya Kamati ya Wataalamu na Kamati ya Usalama ya Mkoa yaliyotolewa kuhusiana na miradi ya maendeleo na maandalizi ya Mbio za Mwenge katika Mkoa wa Mara.
Katika ziara hiyo, Kamati ya Usalama ya Mkoa iliambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Rorya, baadhi ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na maafisa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na viongozi wa taasisi za umma na wasimamizi wa miradi iliyotembelewa.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kupokelewa Mkoa wa Mara tarehe 26 Julai, 2024 na kukimbizwa katika Halmashauri zote tisa kabla ya kukabidhiwa Mkoa wa Simiyu tarehe 4 Agosti, 2024.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa