Kamati ya Usalama wa Mkoa wa Mara inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo imeanza ziara ya kutembelea na kukagua miradi itakayofikiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 kwa kufanya ziara Halmashauri ya Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Kamati hiyo ikiwa katika Manispaa ya Musoma, imetembelea na kukagua jengo la kupumzika abiria katika eneo la Mwigobero lililojengwa na Wakala wa Umeme na Ufundi (TEMESA) na baadaye kuwasalimia na wananchi waliokuwa wamepanda kivuko tayari kuelekea eneo la Kinesi, Wilaya ya Rorya.
Kamati hiyo pia ametembelea na kukagua Zahanati ya Mshikamano ambayo ujenzi wake ulianzishwa kwa nguvu za wananchi na baadaye Serikali kuu na Halmashauri kukamilisha ujenzi huo na kutembelea daraja la Ngaranjabo linalounganisha Kata ya Buhare na Kata ya Makoko linalojengwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
Baada ya hapo, Kamati imeelekea Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambapo ametembelea na kukagua ujenzi wa Zahanati ya Mmahare, ujenzi wa mradi wa maji wa Chumwi Mabuyi unaotekelezwa na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA).
Katika ziara hiyo, Mhe. Mtambi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuyafanyia kazi maekelezo ya Kamati ya Wataalamu na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara kuhusu marekebosho yanayohitaji kufanyika katika miradi yote itakayotembelewa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024.
Wakati huo huo, akiwa katika tenki la mradi wa maji wa Chumwi Mabuyi, Mkuu wa Mkoa wa Mara ameagiza kukarabatiwa kwa Shule ya Msingi Mabume Rafuru ambayo ipo jirani na tenki la mradi wa maji wa Chumwi- Mabuyi ambayo ina majengo mengi yaliyochakaa sana na mazingira yasiyoridhisha.
Mhe. Mtambi ameelekeza sehemu ya mchango wa mwenge wa Wilaya ya Musoma kukarabati shule hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha ofisi ya walimu na kuweka samani katika ofisi ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo na kubomoa vyoo vya zamani ambavyo havitumiki vilivyopo katika eneo hilo kwa kuwa ni hatarishi kwa watoto na vinachafua mazingira.
Mhe. Mtambi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuongeza nguvu katika ukarabati wa shule hiyo na kuhakikisha ukarabati huo unakamilika ili wanafunzi wajivunie kufikiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru katika shule yao.
Kanali Mtambi ameitaka Kamati ya Wataalamu ya Ukaguzi wa Miradi ya Mwenge Mkoa wa Mara kukagua maendeleo ya ukarabati wa shule hiyo tarehe 21 Julai, 2024 na kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa maagizo hayo.
Katika ziara hiyo, Kamati ya Usalama ya Mkoa iliambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Musoma, baadhi ya maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Wakuu wa Taasisi na baadhi ya maafisa wa Halmashauri za Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa