Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imehitimisha ziara yake ya siku tano katika Mkoa wa Mara kwa kufanya ziara katika Wilaya ya Butiama ambapo pamoja na mambo mengine imetembelea Kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Ikiwa katika Wilaya ya Butiama kamati hiyo imeitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kamgegi na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama inayoendelea kujengwa katika wilaya hiyo.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho, Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC Mhe. Stanslaus Mabula ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kutengeneza upya sakafu ya madarasa na milango ya shule hiyo na kuweka mipira chini ya meza na viti ili visiendelee kuharibu sakafu na kumwita Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua.
“Changamoto ninayoiona hapa ni kwamba palikuwa na usimamizi mbovu wa ujenzi tangu fedha zilizopokelewa mpaka sasa, hakukufanyika uchunguzi wa udongo kabla ya kuanza ujenzi, hakukuwa na mpango wa manunuzi katika mradi huu” amesema Mhe. Mabula.
Aidha, Mhe. Mabula amepongeza ujenzi wa nyumba ya walimu (two in one) ambayo amesema imejengwa vizuri kwa vinago vinavyokubalika na ameitaka Halmashauri hiyo kuendelea kutenga fedha kutoka mapato ya ndani ili kukamilisha maabara ya shule hiyo ili wanafunzi waweze kujifunza kwa vitendo.
Kuhusu Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Mhe. Mabula ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kutoa fedha za ukamilishaji wa hospitali hiyo mapema iwezekanavyo kwa kulingana na hadhi ya hospitali hiyo inayojengwa nyumbani kwa Baba wa Taifa.
“Fedha iliyotolewa katika hospitali hii ni kidogo ukilinganisha na hospitali nyingine za Halmashauri, lakini hapa ni nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, panahitaji jicho la kipekee katika kuwapa mgao” amesema Mhe. Mabula.
Aidha, Mhe. Mabula ameutaka uongozi wa Mkoa wa Mara kuisaidia Halmashauri kumbana mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga jengo la wagonjwa wa dharura (EMD) katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ili arejeshe fedha baada ya kuwa amelipwa fedha yote na mkataba wa kazi hiyo kuvunjwa kabla hajakamilisha kazi katika ujenzi wa jengo hilo.
Akitoa ufafanuzi wa hoja za wabunge kuhusu Shule ya Sekondari ya Kamgegi, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Bwana Chacha Megewa ameeleza kuwa kabla ya Serikali haijaleta fedha za SEQUIP katika kata hiyo, tayari wananchi wa Kata hiyo walianzisha ujenzi wa madarasa sita na matundu ya vyoo 10 katika eneo hilo.
“Madarasa haya na matundu ya vyoo Serikali kupitia mpango wa lipa kwa matokeo iliyakamilisha na kuanza kutumika isipokuwa madarasa matatu ambayo kwa sasa yanatumika kama stoo ya kuwekea vifaa na jiko la kupikia chakula cha wanafunzi” amesema Bwana Megewa.
Bwana Megewa amewashukuru wananchi wa Kata hivo kwa michango yao ya hali na mali katika ujenzi wa madarasa hayo na matundu 10 ya vyoo ambayo yameongeza miundombinu ya kutolea elimu katika shule hiyo.
Ziara hiyo imehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Katibu Tawala wa Wilaya ya Butiama, wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, maafisa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Ziara hiyo imehitimishwa kwa wajumbe wa kamati kutembelea Kaburi la Baba wa Taifa katika eneo la Mwitongo, Wilaya ya Butiama kabla ya kuanza safari ya kuelekea Halmashauri ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu kuendelea na ziara yake.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa