Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili imelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kazi nzuri waliyoifanya tangu walipokabidhiwa kazi ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Rwangwa inayoendelea kujengwa katika Manispaa ya Musoma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo tarehe 17 Machi 2020 wajumbe wa kamati hiyo wamepongeza jitihada iliyofanyika tangu NHC wapewe jukumu hilo hadi sasa.
“Kumekuwa na wakandarasi wengi waliofanya hii kazi tangu hospitali hii ilipoanza kujengwa mwaka 1977 lakini kazi yenu inaonekana, hongereni sana, alisema Mheshimiwa Nape Nnauye, Mbunge wa Mtama.
Wakichangia maoni yao wajumbe wa kamati hiyo wameelezwa kuridhishwa kwao kwa namna hatua ya ujenzi ilipofikia na kazi ambayo NHC kama mkandarasi imefanya katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi Nyumba Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi akizungumza wakati wa utambulisho ameeleza kuwa NHC imekuwa ikifanya vizuri katika miradi yote ya kimkakati iliyopewa.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa machinjio ya kisasa jijini Dar es Salaam, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara na mingineyo.
Mheshimiwa Lukuvi amesema mradi huu pia umechelewa kutokana na kuchelewa kupatikana kwa Mshauri Mwelekezi ambaye kwa sasa amepatikana ambaye ni Chuo Kikuu cha Ardhi na anafanyakazi nzuri kwa ushirikiano na NHC.
Hata hivyo amerudia agizo lake la kuitaka NHC kutekeleza ahadi ya kukamilisha upande wenye wodi za Mama na Mtoto na majengo ya mochwari na sehemu ya kufulia katika hospitali hiyo ili ziweze kutumika ifikapo tarehe 17 Aprili 2020.
“Mkurugenzi wa NHC ninaomba kukuambia kuwa kama mradi huu haijakamilika kama tulivyoahidiana ninaomba barua ya kuondoka ofisini uiandike wewe mwenyewe, maana wewe ndio uliahidi utakamilisha ifikapo muda huo” alisema Mheshimiwa Lukuvi.
Wakati huo huo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Vincent Naano Anney ameipongeza NHC kwa kazi kubwa wanayoifanya hususan ya usimamizi mzuri wa mradi huo.
“Wale wakandarasi wa mwanzo ilikuwa kila siku hapa kulikuwa na kesi za wizi wa vifaa, kwa sasa hamna wizi tena wa kiholelaholela, wanajitahidi sana” alisema Dkt. Anney.
Wakiwa katika eneo hilo wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipata nafasi ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo, kupokea taarifa ya ujenzi na kupokea taarifa ya ukaguzi wa mipaka kati ya Kenya na Tanzania.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa