Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani leo tarehe 6 Juni 2020 amezindua vituo vya mafuta vya serikali vyenye lengo la kusogeza huduma za nishati karibu na maeneo ya wananchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo mjini Musoma Mheshimiwa Kalemani alisema kwa leo anazindua vituo saba vinavyomilikiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kupitia kampuni yake tanzu ya TANOIL hapa nchini vikiwa na lengo la kuimarisha na kusogeza huduma za nishati kwa wananchi.
“Serikali imeamua kurudi katika biashara ya mafuta kupitia TPDC na kampuni tanzu ya TANOIL ikiwa ni hatua muhimu kwa usalama na ustawi wa taifa letu” alisema Mheshimiwa Kalemani.
Mheshimiwa Kalemani ameeleza kuwa kwa sasa serikali inazindua vituo saba vya TANOIL nchi nzima na huu ni utekelezaji wa Sera ya Nishati yenye lengo la kupeleka huduma hiyo kwa wananchi.
Aidha Mheshimiwa Kalemani ameuagiza uongozi wa TPDC kuhifadhi mafuta mengi wakati huu ambako bei ya mafuta duniani imeshuka ili kuweza kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta bei itakapopanda katika soko la dunia.
Pia Msheshimiwa Kalemani ameutaka uongozi wa TPDC kufungua vituo vya mafuta viwe vingi hapa nchini ili kuweza kusambaza huduma hizo kwa wananchi walio wengi waweze kunufaika na huduma hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amepongeza Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa walioifanya ya kurudi katika biashara ya mafuta kupitia TPDC.
“Nilikuwa kiongozi katika Wizara ya Nishati na Madini wakati huo na mpango wa TPDC kurudi katika biashara ya mafuta ilikuwepo ni furaha kuona mipango ile kwa sasa inatekelezwa” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha Mheshimiwa Malima alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli ya serikali nzima kwa kutekeleza suala hili muhimu kwa maendeleo ya Taifa la Tanzania.
Akizungumza wakati wa kutoa taarifa kwa Mheshimiwa Waziri, Mkurugenzi Mkuu wa TPDC Dkt. James P. Mataragio ameeleza kuwa TPDC inampango wa kushirikiana na Halmashauri zote hapa nchini ili kufungua vituo vya mafuta katika kila halmashauri hapa nchini.
“Kwa kuanzia katika kipindi cha miaka 5 ijayo TPDC inampango wa kufungua vituo vipya 100 vitakavyokuwa katika halmashauri mbalimbali hapa nchini ili kuendelea kusogeza huduma za nishati kwa wananchi. Alisema Dkt. Mataragio.
Dkt. Mataragio alisema ufunguzi wa vituo hivi utaisaida serikali katika kupanua uwigo wa kodi, kuongeza ubora wa bidhaa, kupanua ajira kwa vijana, na uhakika wa upatikanaji wa mafuta wakati ambapo kuna changamoto.
Ametoa mfano wa miaka ya 1980 TPDC ilikuwa ndio msambazaji mkuu wa mafuta kwa wapiganaji wa msari wa mbele wakati wa vita vya Uganda na Tanzania maarufu kama vita vya Kagera baada ya wasambazaji wengine wa mafuta kugoma kufanya hivyo.
“Kwa niaba ya TPDC ninashukuru sana kwa ushirikiano ambao tumekuwa tukipata kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara wakati wote tangu vituo hivi vilipojengwa mwaka 1978 hadi sasa” alisema Dkt. Mataragio.
Shirika la TPDC lilijenga vituo saba vya mafuta katika mikoa ya kimkakati hapa nchini na kufanya biashara ya mafuta kuanzia miaka ya 1978 hadi 2000 TPDC kupitia kampuni yake ya Tipper. Katika Mkoa wa Mara kupitia mpango huo TPDC ilikuwa na vituo vya mafuta viwili ambavyo vipo katika Manispaa ya Musoma na Mji wa Tarime.
Uzinduzi wa kituo cha Mafuta cha TANOIL Musoma ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima, Naibu Waziri wa Nishati Mheshimiwa Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Meya wa Mji wa Musoma na Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma pamoja na viongozi wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa