Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 822 Rwamkoma kimeibuka mshindi katika mashindano ya Nyama Choma Festival yaliyofanyika leo katika mnada wa Kiabakari, Wilaya ya Butiama na kuhusisha wachomaji nyama mbalimbali kutoka Mkoa wa Mara.
Akitangaza matokeo ya mashindano hayo, Mwenyekiti wa Majaji katika mashindano hayo Bwana Edger Mwansasu amewataja washindi wengine kuwa ni Bwana Deus John aliyeshika nafasi ya pili na Rama Hoteli ambayo imeshika nafasi ya tatu katika mashindano hayo.
Bwana Mwansasu amewataja washindi wengine kuwa ni Bwana John John ambaye ameshika nafasi ya nne huku Meeting Point ikiwa imeshika nafasi ya tano katika mashindano hayo.
Bwana Mwansasu amesema Mshindi wa kwanza amezawadiwa shilingi 500,000, mshindi wa pili 300,000, mshindi wa tatu shilingi 150,000 wakati washindi wote kuanzia namba moja hadi 15 wamejishindia fulana.
Kwa mujibu wa Bwana Mwansasu washiriki katika mashindano hayo walikuwa 32 ambao walitoka katika Wilaya zote za Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Bwana Ramadhani Mkune mmoja ya wachoma nyama katika mnada huo ameishukuru Serikali kwa kuanzisha mashindano hayo ambayo amesema yanatoa fursa kwa wananchi na hususan vijana kujitafutia pesa kwa kufanya kazi halali.
Bwana Mkune ameeleza kuwa kwa kuuza nyama wanayochoma katika mnada huo wanapata faida ambayo inawawezesha kujikimu kimaisha hata hivyo ameitaka Serikali kuwafikiria kuwapa mikopo ili waweze kuanzisha biashara za kuchoma nyama.
Kwa upande wake, Meneja wa Tanzania Commercial Benki, Tawi la Musoma Bwana Edward Emmanuel ambaye ni moja ya wadhamini wa mashindano hayo, amesema wananshukuru sana kuwa sehemu ya mashindano hayo na kuahidi kuendelea kudhamini mashindano hayo yakifanyika wakati mwingine.
Bwana Emmanuel ameomba waandaaji wa mashindano haya kuyafanya siku za Jumamosi ili kuwavutia washiriki wengi zaidi wa kutoka nje ya Mkoa wa Mara waweze kufika na kufurahia utofauti uliopo katika nyama choma ya Mkoa wa Mara.
Mashindano hayo yamedhaminiwa na Benki ya Posta, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo, Umoja wa Wachimbani wa Dhahabu wa Irasanilo, container park na kadhalika.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa