Mkuu wa Majeshi Mtaafu, Jenerali David Bugozi Musuguri anatarajiwa kuzikwa kwa heshima za kijeshi nyumbani kwake katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Butiama, Mkoa wa Mara Jumatatu tarehe 04 Oktoba, 2024.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda imeeleza kuwa Jenerali Musuguri (104) amefariki jana tarehe 29 Oktoba, 2024 katika Hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza wakati akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dotto Mashaka Biteko anatarajiwa kuongoza zoezi la utoaji wa heshima za mwisho za kijeshi kesho tarehe 01 Novemba, 2024 katika Hospitali Kuu ya Jesho Lugalo Jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa marehemu alizaliwa tarehe 04 Januari, 1925) katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma (kwa sasa Butiama) na kupata elimu katika ngazi mbalimbali.
Marehemu alijiunga na Jeshi tarehe 09 Agosti, 1943 na kuhudhuria kozi na mafunzo mbalimbali katika nchi za Kenya na China na wakati wa uhai wake alilitumikia Jeshi kwa zaidi ya miaka 45 hadi alipostaafu jeshini kwa heshima tarehe 01 Septemba, 1988.
Kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika kulitumikia Jeshi na kulinda Taifa, Rais na Amiri Jeshi Mkuu alimtunuku medali mbalimbali ikiwa ni pamoja na medali ya Vita vya Kagera, Miaka 20 ya JWTZ, Utumishi Mrefu Tanzania na Utumishi Uliotukuka Tanzania.
Sekretarieti ya Mkoa wa Mara inatoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki waliofikwa na msiba huu, Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa