Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Mheshimiwa Dkt. Suleiman Jafo (Mb.) ameunda Kamati ya Kitaifa ya watu 11 kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa maji ya Mto Mara.
Akizungumza baada ya kutembelea Mto Mara katika eneo la Kirumi na kupokea taarifa kutoka kwa viongozi, wananchi na wataalamu, Mheshimiwa Jafo ameitaka Kamati hiyo kufanya uchunguzi wa maji ya mto huo na kutoa taarifa ndani ya siku saba (7) kuanzia leo tarehe 12 Machi, 2022.
“ Mbali na kufanya uchunguzi wa maji ya Mto Mara ifanye uchunguzi wa maji yote kandokando ya mto huo ili kuona kama kuna uchafuzi wa namna hiyo na kutoa mapendekezo ya kitaalam ili kukabiliana na uchafuzi huo” alisema Mheshimiwa Jafo.
Mheshimiwa Jafo amemtaja Mwenyekiti wa Kamati hiyo kuwa ni Prof. Samwel Manyele, kutoka Idara ya Uhandisi wa Kemikali na Madini, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Katibu wa Kamati hiyo ni Dkt. Samuel G. Mafwenga, Mkurugenzi Mkuu, Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Wajumbe wa kamati hiyo ni pamoja na Dkt. Kessy F. Kilulya, Mkuu wa Idara ya Kemia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Charles Kasanzu, kutoka Idara ya Jiolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bwana Daniel Ndio, Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali, Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Bwana Renatus Shinhu, Mkurugenzi wa Bonde, Mamlaka wa Bonde la Maji Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Jafo amewataja wajumbe wengine kuwa ni Bi. Baraka Sekadende, Mkurugenzi wa Kituo, Taasisi ya Utafiti wa Samaki (TAFIRI), Mwanza, Dkt. Neduvoto Mollel, kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Usimamizi wa Viatilifu (TPHPA), Afisa kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Bwana Yusuf Gobe Kuwaya kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Faraja Ngelageza, Mkurugenzi Msaidizi Bioanuai, kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mheshimiwa Jafo amesema kutokana na uchafuzi huo, maji yamebadilika rangi, yanatoa harufu na samaki aina ya sato wamekuwa wanakufa na kuelea katika Mto huo.
Mheshimiwa Jafo amewataka wananchi, Serikali na wadau wote kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati hiyo katika kipindi chote watakachokuwa wanafanya uchunguzi wa jambo hilo.
Aidha, Mheshimiwa Jafo ameitaka Mamlaka ya Maji Vijijini (RUWASA) kutafuta mbadala wa upatikanaji wa maji kwa wananchi waliopo kandokando ya Mto Mara wakati uchunguzi ukiwa unaendelea. Vilevile, amewataka wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikiwa inalifanyia uchunguzi tatizo hilo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Msovela amempongeza Mheshimiwa Jafo kwa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na uchafuzi wa Mto Mara.
“Viongozi na wataalamu wote wa Mkoa wa Mara tutatoa ushirikiano kwa Kamati hii ili iweze kutekeleza majukumu yake na kutoa matokeo haraka iwezekanvyo” alisema Bwana Msovela.
Mkutano wa Mheshimiwa Jafo ulihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelis Mafumiko, Wakuu wa Wilaya za Rorya, Tarime na Butiama, wataalamu kutoka taasisi mbalimbali zinazohusiana na Maji, Mazingira na Barabara.
Mto Mara unatiririsha maji yake kutoa katika milima ya Mau iliyopo nchini Kenya na baadaye kuingia Tanzania katika Wilaya za Serengeti, Tarime, Butiama na Rorya kabla ya kuingiza maji yake katika Ziwa Victoria.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa