Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mheshimiwa Suleiman Jafo amesikitishwa na ubabaishaji unaofanywa na Mgodi wa North Mara uliopo katika Wilaya ya Tarime, Mkoani Mara katika utekelezaji wa maagizo ya serikali katika kulinda mazingira.
Mheshimiwa Jafo ameeleza masikitiko yake leo tarehe 20 Aprili 2021 wakati akiwa katika ziara ya siku moja Mkoani Mara kutembelea mgodi huo ili kujua hatua za utekelezaji wa maagizo ya serikali.
“Leo mimi nilitegemea wangesema kuwa tumechukua hatua kadhaa na sasa tunategemea kuondokana na tatizo la mlundikano wa maji yenye sumu kwa ifikapo mwezi fulani, lakini haya maelezo yao hayaonyeshi nia ya kuondokana na tatizo hili” alisema Mheshimiwa Jafo.
Kufuatia hali hiyo Mheshimiwa Jafo ametoa siku saba kwa mgodi wa North Mara kuwasilisha taarifa ofisini kwake kuhusu mkataba wao na mkandarasi unaoonyesha ni lini upembuzi yakinifu na muundo wa mfumo mpya wa maji taka utakamilishwa pamoja na mpangokazi wa kutekeleza maagizo ya serikali.
Mheshimiwa Jafo alisema awali mgodi huu ulikuwa unazalisha maji taka kiasi cha lita za ujazo 7,000,000 kwa sasa wamejitahidi kupunguza wamefikia lita milioni 2.2 hata hivyo bado hayakubaliki kwani Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linataka maji hayo yabakie lita 800,000 ili kulinda afya za wananchi wanaouzunguka mgodi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameeleza kuwa suala la kuhifadhi maji machafu ili yasiwaathiri wananchi limekuwa likiongelewa na serikali kwa muda mrefu lakini mgodi hauchukui hatua za kukomesha hali hiyo.
“Nafahamu kuwa serikali inaubia na mgodi wa Barrick katika uendeshaji wa migodi hii, lakini sisi (serikali) hatuna ubia wowote na mgodi kwenye ulinzi na usalama wa watanzania na mali zao na hatutaki utani kwenye suala nyeti kama hili” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa hata sehemu ambayo North Mara wanasema wameshaitenga kwa ajili ya kujenga bwawa jipya bado mgodi haujalipa fidia kwa wananchi wenye eneo hilo na kama serikali ya Mkoa inasubiri kuona utekelezaji huo.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa hii ni mara ya tatu sasa anafika hapo na mawaziri tofauti wa mazingira kufuatilia jambo hilo lakini wamekuwa wakipewa maelezo ambayo hayaridhishi juu ya utekelezaji wa maagizo hayo.
Awali akitoa maelezo kwa Mheshimiwa Waziri, Msimamizi wa Bwawa hilo Bwana Majuto Kapande ameeleza kuwa kwa sasa upembuzi yakinifu kuhusu mradi huo unaendelea hata hivyo alishindwa kutaja tarehe ya kukamilika kwa upembuzi huo.
“Ni kweli tunalifanyia kazi na kwa sasa tayari mgodi umempa kazi mshauri mwelekezi kutoka Afrika Kusini ambaye anafanya upembuzi yakinifu pamoja na kuandaa michoro na muundo wa bwawa jipya litakalojengwa” alisema Bwana Kapande.
Hata hivyo Bwana Kapande na wenzake waliokuwa katika msafara huo walishindwa kueleza kuhusu mkataba wao na mkandarasi huyo ulianza lini, unaisha lini na bwawa litaanza kujengwa lini jambo ambalo lilileta wasiwasi kuwa huenda hamna utekelezaji wowote unaoendelea.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa