Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) leo tarehe 25 Agosti, 2024 imefanya mkutano na wadau wa uchaguzi Mkoa wa Mara na kuvionya vyama vya siasa kutokuingilia mchakato wa uboreshaji wa Daftari la wapiga kura.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Tume Huru la Uchaguzi Jaji Mahakama ya Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele amesema mawakala na viongozi wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuingilia mchakato wa uandikishaji vituoni na kufanya hivyo watakiuka Sheria za Uchaguzi.
“Kila Chama cha siasa kimepewa nakala ya orodha ya vituo vyote vya kuandikisha wapiga kura ili kuwawezesha kupanga kupanga na kuweka mawakala wa uandikishaji katika vituo vya kuandikisha wapiga kura” amesema Jaji Mwambegele.
Mhe. Jaji Mwambegele amevihimiza vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni za uboreshaji, maelekezo ya Tume na kusimamia miiko na mipaka ya uendeshaji wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura.
Amevitaka vyama vya siasa kutumia sheria zilizopo kuwasilisha changamoto zinazojitokeza kwa Tume na kuongeza kuwa INEC itazingatia Katiba, Sheria za Uchaguzi na kanuni zilizotungwa chini ya Sheria katika zoezi la uboreshaji.
Jaji Mwambegele amewataka wadau wa uchaguzi kuwa mabalozi wazuri na kutoa taarifa sahihi kwa wananchi na kuwahamasisha wananchi wenye sifa kujitokeza kwa wingi na kuboresha taarifa zao ili zoezi hili lifanyike kwa ufanisi na mafanikio makubwa.
Jaji Mwambegele amesema katika mzunguko wa nne wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utahusisha mikoa ya Mara, Simiyu, na sehemu ya Mkoa wa Manyara katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Mji wa Babati ambapo uboreshaji utaanza tarehe 4-10 Septemba, 2024.
Amesema vituo vya kujiandikisha vitafunguliwa kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni na kuwataka wadau wa uchaguzi katika mikoa hiyo watatakiwa kuwawapa taarifa sahihi wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC Bwana Ramadhani Kailima amesema Tume inategemea vyama vyenye usajiri kamili kutumia fursa za kisheria zilizotolewa kwao kuhakikisha kuwa zoezi la uboreshaji linafanikiwa na kuongeza kuwa endapo kutajitokeza changamoto zozote vyama vitumie taratibu za kisheria zilizopo kuwasilisha hoja zao.
“Viongozi wa vyama vya siasa hawapaswi kuingilia utekelezaji wa majukumu ya watendaji wa vituo wakati wote wa uandikishaji wa wapiga kura vituoni kama kuomba orodha au idadi ya walioandikishwa au kuboresha au kuhamisha taarifa zao” amesema Bwana Kailima.
Bwana Kailima amesema Tume inao wajibu wa kuwapatia viongozi wa vyama vya siasa taarifa kamili ya zoezi la uandikishaji wa Daftari la Wapiga Kura mara baada ya zoezi kukamilika.
Kauli mbiu ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mwaka 2024/2025 ni “Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora”.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa, wahariri wa vyombo vya habari za kijamii vilivyopo Mkoa wa Mara, wawakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii na wawakilishi wa taasisi za Serikali Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa