Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) kupitia mradi wake wa utafiti wa kichaa cha mbwa imepanga kuupatia Mkoa wa Mara chanjo ya kichaa cha mbwa kwa muda wa miaka mitano na miundombinu kwa jumla ya zaidi ya shilingi milioni 400.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha matokeo ya awali ya utafiti wa mikakati ya kudhibiti kichaa cha mbwa kwa viongozi na watendaji wa Mkoa wa Mara, Mratibu wa Programu ya Kudhibiti Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa Dkt. Ahmed Lugelo ameeleza kuwa msaada huo ni sehemu ya mwendeleo wa mradi wa kudhibiti kichaa cha mbwa katika Mkoa wa Mara.
“Tutatoa chanjo zenye thamani za zaidi ya shilingi milioni 116 kwa kipindi cha miaka mitano na kwa mwaka huu tutaweka miundombinu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 279 kwenye kata zilizokuwa kwenye mpango mpya wa majaribio” amesema Dkt. Lugelo.
Kwa mujibu wa Dkt. Lugelo, chanjo pamoja na vifaa tiba vitaletwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na ofisi hiyo itaratibu zoezi la chanjo hiyo kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara ameseka Dkt. Lugelo.
Dkt. Lugelo ameeleza kuwa tangu mradi huu wa utafiti ulipoanza mwaka 2019, Taasisi ya Afya ya Ifakara kwa kushirikiana na wadau wengine imekuwa ikitoa chanjo ya kichaa cha mbwa katika Mkoa wa Mara bila malipo.
Aidha, Bwana Lugelo ameeleza kuwa wakati wa utafiti huo zaidi ya mbwa 220,000 wamechanjwa katika Mkoa wa Mara na mradi huo pia umetengeneza kifaa cha kuhifadhia chanjo ambacho hakitumii umeme na tayari kimefanyiwa vipimo kinafaa kwa matumizi.
Dkt. Lugelo ameeleza kuwa mradi huo wa miaka mitatu ulianza Oktoba, 2019 na unatarajiwa kuisha tarehe 30 Oktoba, 2023 na umefanyakazi katika Kata 132 katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara
Dkt. Lugelo ameeleza kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa unaenea kutoka kwa mbwa kwenda kwa binadamu na wanyama wengine kwa haraka na kwa binadamu chanjo yake inatolewa baada ya mtu kung’atwa na mbwa chanjo hiyo ni ya gharama kubwa na hauna dawa za kuweza kuutibu ugonjwa huo baada ya dalili kuonekana.
Dkt. Lugelo amewashukuru viongozi na watendaji wa Mkoa wa Mara walioshiriki katika kikao hicho na kuwataka watoe elimu kuhusu madhara ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa katika jamii na mwakani mwezi Oktoba, 2023 taasisi hiyo itafanya mkutano wa tathmini kuhusiana na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa leo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda ameipongeza Taasisi ya Afya Ifakara kwa kuleta mradi huo katika Mkoa wa Mara na kutoa msaada wa chanjo ya Kichaa cha Mbwa pamoja na miundombinu itakayorahisisha udhibiti wa kichaa cha mbwa.
Mhe. Mtanda amezitaka Halmashauri zote kutafuta namna ya kudhibiti mbwa kuzurura mitaani ili kuondoa hofu kwa wananchi ya kung’atwa na mbwa wenye kichaa cha mbwa.
Kwa upande wao, washiriki wa kikao hicho wameamua kuwa ili kunufaika na msaada huo, Halmashauri zitenge bajeti ya kusaidia kudhibiti kichaa cha mbwa na wananchi wachangie shilingi 500 kwa kila mbwa atakayepatiwa chanjo kwa kipindi hicho.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Meya na Wenyeviti wa Halmashauri, Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wakurugenzi na watendaji kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa