Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kwangwa inatarajia kuanza kutoa huduma katika Jengo la Mama na Mtoto kuanzia tarehe 17 Aprili 2020 baada ya kukamilika ujenzi wa upande huo na huduma zote muhimu za kuwezesha kuanza kufanya kazi.
Hayo yameelezwa leo baada ya kikao cha pamoja kati ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kigoma Malima, wawakilishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambao ndio wakandarasi na mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Ardhi ambaye ni Mshauri Mwelekezi katika mradi huo pamoja na maafisa waandamizi wa serikali.
Akizungumza baada ya kikao hicho Mheshimiwa Lukuvi ameeleza kuwa amewaagiza NHC kuhakikisha kuwa wanafanyakazi ya kukamilisha ujenzi wa hospitali hii kwa usiku na mchana na kuhakikisha kuwa huduma zitaanza kutolewa kwa muda uliopangwa.
“Kwa sasa Mshauri Mwelekezi anarekebisha michoro ya awali ya majengo hayo ili iweze kukidhi mahitaji yote ya msingi ya majengo ya wakati huu” alisema Mheshimiwa Lukuvi.
Kwa upande wake Mheshimiwa Mwalimu amesema kuwa wanategemea kuwa hospitali hii itaanza kufanyakazi kwa kutoa huduma za mama na mtoto na makubaliano ni kuwa hadi kufikia Julai, 2020 hospitali yote itakuwa imekamilika kutoa huduma kwa wananchi.
“Tunategemea kuwa ujenzi huu ukikamilika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara itahamia hapa Kwangwa na pale ilipo sasa yale majengo yatatumika kama Hospitali ya Manispaa ya Musoma” alisema Mheshimiwa Mwalimu
Aidha amesema kuwa hospitali hii haitakuwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa bali itakuwa ni hospitali ya kibingwa na kibobezi kwa baadhi ya huduma na itatoa huduma kwa wananchi wote wa Kanda ya Ziwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Adam Kighoma Malima amesema kuwa ziara ya viongozi hawa imesadia sana katika kutatua changamoto zilizokuwa zinaukabili ukamilishaji wa hospitali hii.
Ujenzi wa Hospitali ya Kwangwa ulianza mwaka 1977 na ulikuwa ukijengwa taratibu hadi mwaka 2018 ambapo Rais wa awamu ya tano Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli alipoamua kutoa shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kumalizia ujenzi huu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa