Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara inatarajiwa kuhamia katika majengo ya Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo katika eneo la Kwangwa tarehe 01 Julai, 2023.
Akizungumza katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Mara na Wazee wa Manispaa ya Musoma, Bwana Msalika amesema kuhama kwa hospitali hiyo kutatoa nafasi wa majengo yaliyokuwa wakitumiwa na hospitali hiyo kutumika kama Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.
“Maandalizi yote muhimu yamekamilika, hospitali ya Rufaa na Hospitali ya Halmashauri zimeshasajiriwa rasmi na zote zipo tayari kwa ajili ya kupokea wagonjwa” amesema Bwana Makungu.
Kwa mujibu wa Bwana Makungu katika kuhakikisha huduma hazisimami katika hospitali ya awali, baadhi ya vifaa tiba, dawa na watumishi wataendelea kubaki kuhudumia wagonjwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma ili huduma ziendelee kutolewa.
Aidha, Bwana Makungu amesema tayari Manispaa ya Musoma imepokea fedha shilingi milioni 500 ambazo zitatumika katika kukarabati majengo yaliyokuwa yakitumika na Hospitali ya Rufaa ili yaweze kutumika na Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.
Bwana Makungu amewahakikishia wazee wa Manispaa ya Musoma kuwa zoezi la uhamaji limewekewa taratibu ambazo hazitaathiri utoaji wa huduma za Hospitali ya Manispaa ya Musoma wakati kwa hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere maboresho yanaendelea.
Ameyataja maboresho yanayoendelea kuwa ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za maji katika Hospitali ya Rufaa jambo linaloshughulikiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) na ujenzi wa vyoo vya nje kwa watu wanaokuja kuona wagonjwa vinavyosimamiwa na Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma.
Wakati huo huo, Bwana Makungu amesema iliyokuwa Musoma Hoteli inatarajiwa kufufuliwa baada ya mwekezaji mwenye asili ya Mkoa wa Mara kuonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika Hoteli hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Musoma Mhe. Magiri Benedicto Malegesi ameitaka Serikali kukipanua Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare ili kiweze kuchukua programu nyingi na kutoa shahada za kwanza.
“Kwa sasa Chuo kina wanafunzi 900 tu, wakiongeza michepuo na wakianza kutoa Shahada kitaongeza idadi ya wanafunzi na hilo litaisaidia sana katika kukua kwa Manispaa ya Musoma” alisema Mhe. Malegesi.
Mhe. Malegesi ameiomba Serikali kufufua viwanda vya zamani na kujenga viwanda vipya ili kuongeza ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.
Wengine walioshiriki katika mazungumzo hayo Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya, Ustawi wa Jamii na lishe Dkt. Zabron Masatu, Meya wa Manispaa ya Musoma Mhe. Wiliam Gumbo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Bwana Bosco Ndunguru.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa