Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara inatarajiwa kuanza kutoa huduma zake zote katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo katika eneo la Kwangwa na kuachia majengo inayoyatumia sasa kwa ajili ya Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.
Hayo yameelezwa leo tarehe 28 Septemba, 2022 katika Kikao cha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe na wadau wote muhimu wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
“Wizara ya Afya inataka hospitali hii ianze kutoa huduma zake zote hapa Kwangwa haraka iwezekanavyo, hilo linawezekana kama kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake katika kuhakikisha kuwa Hospitali hii inahamia hapa ifikapo tarehe 15 Desemba, 2022 na tunaamini kwa hatua ya ujenzi iliyofikia hili linawezekana” alisema Dkt. Shekalaghe.
Dkt. Shekalaghe ameeleza kuwa tayari Wizara imetenga shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo katika mwaka wa fedha 2022/2023 pamoja na kununua vifaa tiba muhimu kwa ajili ya hospitali hiyo kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha, Dkt. Shekalaghe amemtaka Mkandarasi wa mradi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukamilisha kazi zilizobakia kwa awamu ya kwanza na kukabidhi kazi tarehe 27 Novemba, 2022 kwa mujibu wa mkataba.
Dkt. Shekalaghe ameeleza kuwa tayari maandalizi yameanza kwa ajili ya Wizara ya Afya kutoa mkataba wa awamu ya pili kwa mkandarasi huyo na mkataba huo unatarajiwa kusainiwa mwishoni mwa Oktoba baada ya taratibu za zabuni kukamilika.
Aidha, Dkt. Shekalage ameeleza kuwa Wizara pia inampango wa kukamilisha jengo la radiolojia ili mashine za CT-Scan na Digital X-ray zilizonunuliwa na Serikali kwa ajili ya hospitali hiyo ziweze kufungwa na kutoa huduma kwa wananchi haraka iwezekanavyo.
Ili kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo kwa haraka, Dkt. Shekalage ameeleza kuwa Wizara imembadilisha aliyekuwa msimamizi wa mradi huo kutoka wizarani (clerk of works) na kuleta mhandisi mwandamizi kutoka Wizarani ili kusimamia mradi huo na kutoa mrejesho wa haraka kwa viongozi.
Dkt. Shekilage ametoa tahadhari kwa wazabuni wote waliopewa zabuni katika mradi huo kutekeleza majukumu katika mradi huo kwa haraka, ubora na kulingana na mikataba yao.
“Hatutamvumilia mzabuni yoyote atakayechelewesha mradi huu kutokana na uzembe, tunataka uwajibikaji na umakini katika utekelezaji wa kazi zenu” alisema Dkt. Shekalage.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Khalfan Haule ameeleza kuwa Hospitali hiyo ikihamia eneo la Kwangwa itaimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Mara na hususan waliopo Manispaa ya Musoma.
Dkt. Haule ameeleza kuwa kwa sasa wagonjwa wa kutoka Wilaya ya Musoma wanapata rufaa kutoka vituo vya afya Kwenda moja kwa moja katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa bila kupitia Hospitali ya Halmashauri jambo ambalo amesema linaongeza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali hiyo.
Hata hivyo Dkt. Haule ameeleza kuwa anatamani kama wazabuni wote waliosaini mikataba ya zabuni wangekuwepo wenyewe kutoa ahadi za kukamilisha ujenzi huo kama walivyofanya Chuo Kikuu cha Ardhi ili kuhakikisha utekelezaji wa haraka wa mradi huo.
Kwa Upande wake, Meya wa Manispaa ya Musoma Mheshimiwa William Gumbo ameeleza kuwa amefurahishwa sana na kikao hicho maana kimetoa mwanga wa lini Hospitali ya Rufaa ya Mkoa itahama katika majengo yanayotumika sasa ili kuweza kuanzisha Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.
“Sasa wananchi wa Musoma wanauhakika wa kupata hospitali yao ambayo itawahudumia kwa viwango nafuu na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika vituo vya afya na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa” alisema Mheshimiwa Gumbo.
Kikao hicho cha kujadili maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Nyerere kilihudhuriwa pia na Mwakilishi wa mkandarasi wa mradi huo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mshauri Mwelekezi (Chuo Kikuu cha Ardhi), wakandarasi wengine wadogo wadogo wa mradi huo, viongozi wa Mkoa wa Mara, Wilaya ya Musoma, Manispaa ya Musoma pamoja na Bodi na Menejimenti ya Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Kwa sasa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imeanza kutoa huduma katika vitengo vya Mama na Mtoto na Magonjwa ya ndani kuanzia mwishoni mwa mwezi Agosti, 2020.
Hospitali hii ikikamilika inatarajiwa kuwa ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Mashariki na kutoa matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali na kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Butiama ambapo programu za afya zitafundishwa hapo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa