Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ambayo ni maarufu kuwa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyojengwa katika eneo la Kwangwa, Manispaa ya Musoma imeanza kutoa huduma kwa wananchi leo tarehe 31 Agosti 2020.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameeleza kuwa kuanza kutolewa huduma katika hospitali hii ni uthubutu wa serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dokta John Pombe Joseph Magufuli aliyetoa msimamo wa kukamilishwa kwa hospitali hii.
“Hospitali hii ilikuwa inajengwa tu awamu zote tangu mwaka 1977, lakini kwa sasa serikali imeamua kuikamilisha na imekamilika na leo imeanza kutoa huduma kwa wananchi, tunashukuru sana” alisema Mheshimiwa Malima.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Malima kwa sasa Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) na Kitengo cha Mama na Mtoto. Aidha ukamilishaji wa shughuli zilizosalia unaendelea ili kuweza kufungua Kitengo cha Magonjwa ya Ndani na kuanza kusafisha figo katika hospitali hii.
“Sisi kama Mkoa tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji mkubwa alioufanya ili kulinda afya za wananchi wa Mkoa wa Mara na maeneo jirani” alisema Mheshimiwa Malima.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Florian Tinuga ameeleza kuwa tayari serikali imeongeza watumishi wengi wa sekta ya afya wakiwemo madaktari ili kuwezesha hospitali hii kuanza kutoa huduma kikamilifu.
“Awali Mkoa ulikuwa na madaktari 34 mwaka 2015 na sasa wameongezeka hadi kufikia madaktari 102 mwaka 2020 na kati ya hao sita ni madaktari bingwa” alisema Dokta Tinuga.
Dokta Tinuga ameeleza kuwa serikali ya awamu ya tano imekamilisha pia hospitali nne za halmashauri za wilaya ambazo ni za halmashauri za wilaya ya Serengeti, Musoma Vijijini, Rorya na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Aidha serikali imejenga vituo vya afya nane katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake mmoja wa wazazi ambaye amejifungua mtoto wake katika hospitali hii Bibi Lucy Msela Nzunda mkazi wa mkazi wa Makoko, alimshukuru Mungu kwa kujifungua salama.
Bibi nzunda amesema huduma katika hospitali hii ni nzuri na wauguzi wamempa ushirikiano na amefurahi sana kuwa mama wa kwanza kujifungua mtoto katika hospitali hii ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Wazo la kujenga hospitali hii lilitolewa na Mwalimu Nyerere mwaka 1975 na ujenzi wa hospitali hii ulianza mwaka 1977 na ulifanywa na wakandarasi mbalimbali na baadae kusimama hadi mwaka 2018 baada ya serikali ya Awamu ya Tano kutoa fedha shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kukamilisha hospitali hii.
Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni kati ya Hospitali 10 za rufaa zilizokamilishwa na serikali ya awamu ya tano kwa usimamizi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika kipindi cha miaka mitano.
Tayari mpaka jana mchana akinamama watatu walikuwa wamejifungua watoto salama katika hospitali hiyo ambapo watoto wawili walikuwa wakike na mmoja wa kiume.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa