Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kujibu hoja zote za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ndani ya mwezi mmoja na zile zenye sura ya jinai ndani yake zipelekwe kwenye vyombo vya dola.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo hayo leo tarehe 14 Julai, 2022 katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo kwa ajili ya kujadili hoja za CAG.
“Hapa tunahoja nyingi ambazo zinajinai ndani yake, sasa tukishindwa kuzijibu tuvikabidhi vyombo vya dola vizishughulikie na wahusika warejeshe pesa ya Halmashauri iliyotumika vibaya” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha ameitaka Halmashauri hiyo kuwashtaki watumishi waliokuwa wanakusanya mapato bila ya kupelekwa benki; waliopewa masurufu ambao wameshindwa kurejesha; walioandika hati kwa mkono kuficha GFS Code; na waliofanya matumizi yasiyo sahihi.
“Ninataka mzabuni aliyelipwa shilingi 292 kwa ajili ya kuleta vifaa vya ujenzi wa ofisi za Halmashauri ambaye hajaleta kwa muda mrefu na waliohusika wote wachukuliwe hatua za kisheria” aliagiza Mheshimiwa Hapi.
Aidha, ameitaka Halmashauri hiyo kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri na kusema “sijaridhika kabisa Halmashauri hii kuishia asilimia 70 ya makusanyo ya ndani, ongezeni juhudi ili miradi ya wananchi iliyopangwa iweze kutekelezwa kwa ufanisi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuongeza wafanyakazi katika Idara ya Mipango mapema iwezekanavyo.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Bunda Bibi Changwa Mkwazu ameeleza kuwa Halmashauri hiyo ilipata hati mbaya katika taarifa kuu, hata hivyo bado haijapokea taarifa ya mradi wa mfuko wa pamoja wa afya (Health Basket Fund).
Bibi Mkwazu ameeleza kuwa halmashauri ilikuwa ina hoja 92 na kati ya hizo hoja 49 ni za miaka ya nyuma wakati hoja 43 ni za mwaka wa fedha 2020/2021.
Bibi Mkwazu ameeleza kuwa kati ya hoja za miaka ya nyuma kuanzia mwaka wa fedha 2012/2013 ambapo hoja 04 zimejibiwa na kufungwa, hoja 16 zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wakati hoja 29 hazijatekelezwa.
Katika hoja za mwaka wa fedha 2020/2021, Bibi Mkwazu ameeleza kuwa hoja 08 zimejibiwa na kufungwa, hoja 27 zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, hoja 07 hazijatekelezwa wakati hoja moja imepitwa na wakati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mheshimiwa Charles Manumbu ameeleza kuwa Halmashauri hiyo imechukua hatua za kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani na sasa inakusanya vizuri.
Mheshimiwa Manumbu ameishukuru Serikali kwa kubadilisha watumishi waliokuwa wamekaa muda mrefu na kuwaleta wengi wapya, hata hivyo ameiomba Serikali kuongeza watumishi katika Idara ya Mipango ya Halmashauri hiyo.
“Ni matumaini yangu, mwakani Halmashauri hii itapata hati safi baada ya wataalamu wengi waliokuwepo kubadilishwa na waliokuja kuonekana wanafanya kazi vizuri” alisema Mheshimiwa Manumbu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa