HAPI: VIONGOZI NA WATUMISHI TUTIMIZE WAJIBU WETU KWA WANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amewataka viongozi na watumishi wa serikali katika Mkoa wa Mara kutimiza wajibu wao kikamilifu ili kuweza kuleta maendeleo yanayotarajiwa kwa wananchi wa Mara.
Mheshimiwa Hapi ametoa kauli hiyo leo katika maeneo mbalimbali baada ya kuwasili na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa serikali, Chama cha Mapinduzi, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, watumishi wa serikali, wazee na viongozi wa mashirika na taasisi za serikali.
“Sisi wote tumetumwa na serikali kuja kuleta maendeleo na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Mkoa wa Mara, kwa hiyo kila mtu kwa nafasi yake tuwajibike kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi, chama ambacho wananchi wamekichagua kuwaletea maendeleo ” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amewataka viongozi na watumishi kutimiza wajibu wao bila ya kusubiri kukumbushwa wala kufuatiliwa na watu wengine ili wananchi waweze kupata manufaa wanayoyatarajia kutoka kwa serikali yao ya Chama cha Mapinduzi.
Aidha amewataka Maafisa Utumishi , wakurugenzi wa halmashauri na wasimamizi wa kazi katika maeneo mbalimbali kutenga muda wa kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa Mkoa wa Mara ili watumishi waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Hapi amewataka viongozi na watumishi wote wa Mkoa wa Mara kushirikiana na kufanya kazi kama timu moja ambayo imeajiriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuweza kuleta maendeleo na kutatua changamoto za wananchi wa Mkoa wa Mara.
“Mimi ninaamini kuwa ushirikiano kati yetu viongozi na watumishi wa serikali na baina ya serikali na Chama na wadau wengine utatusaidia sana katika kutimiza wajibu wetu lakini pia katika kuwaletea wananchi maendeleo yanayohitajika kwa haraka zaidi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Baada ya kuwasili katika Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Hapi alipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mheshimiwa Mwalimu Lyidia Bupilipili, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na viongozi wengine.
Mara baada ya mapokezi hayo Mheshimiwa Hapi ametembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo akiwa hapo amepata nafasi ya kutembelea kaburi la Baba wa Taifa, maktaba binafsi ya Baba wa Taifa pamoja na kuzungumza na viongozi na wazee wa Wilaya ya Butiama.
Akiwa nyumbani kwa Baba wa Taifa Mheshimiwa Hapi amepokelewa na mtoto wa Baba wa Taifa Bwana Madaraka Nyerere, wanafamilia wengine pamoja na wazee na viongozi wa Wilaya ya Butiama.
Baada ya kutoka Butiama, Mheshimiwa Hapi ametembelea na kusaini kitabu cha wageni katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara na kupokelewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Mheshimiwa Samweli Kiboye maarufu kama Namba 3 na viongozi wengine wa CCM Mkoa wa Mara.
Baada ya hapo Mheshimiwa Hapi amezungumza na viongozi na watumishi mbalimbali wa Mkoa wa Mara waliokusanyika kumpokea katika ukumbi wa uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Hapi amehamishiwa Mara kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi ambaye amehamishiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza baada ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko tarehe 11 Juni 2021.
Baada ya uteuzi huo, Mheshimiwa Hapi alishiriki ziara ya Rais aliyoifanya katika Mkoa wa Mwanza akiuwakilisha Mkoa wa Mara na leo amewasili rasmi katika Mkoa wa Mara kutekeleza majukumu yake.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa