Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 21 Juni 2021 amewaapisha Wakuu wa Wilaya wanne wapya walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 19 Juni 2021.
Akizungumza wakati wa kuawaapisha wakuu wa wilaya hao, Mheshimiwa Hapi amewataka kwenda kusimamia miradi ya serikali inayotekelezwa katika wilaya zao ili wananchi waweze kupata manufaa ya miradi hiyo kama ilivyokusudiwa.
“Wananchi wamekipa dhamana Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiamini kitawaletea maendeleo na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili na CCM ikaunda serikali ya Rais aliyewatuma kumwakilisha huku kutatua kero za wananchi wa Mkoa wa Mara, sasa tukachape kazi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amewataka Wakuu wa Wilaya kutumia asimilia 70 ya muda wao wakiwa kwenye kukagua miradi na kusikiliza kero za wananchi na kutumia asilimia 30 tu ya muda wao kukaa ofisini.
“Ninataka mtenge muda na siku maalum mkiwa na wataalamu wenu ili kusikiliza kero za wananchi wa wilaya zenu na kutatua baadhi ya kero za wananchi mtakazoweza na ambazo mtaona mnahitaji msaada kuzitatua tupo tayari kusaidiana kuweza kuzitatua ” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha Mheshimiwa Hapi amewataka viongozi hao kusimamia haki za wananchi wanyonge pamoja na watumishi waliopo katika maeneo yao hususan wanaoishi maeneo ya vijijini .
“Mhakikishe kuwa Maafisa Utumishi wanaenda kuwasikiliza watumishi mbalimbali waliopo katika maeneo yenu, ili watumishi wawatumikie wananchi wakiwa na furaha na wananchi nao wahudumiwe wakiwa na furaha” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amewataka kutilia mkazo zaidi katika sekta za huduma za jamii hususan elimu, afya, maji na umeme ambazo zinawaathiri wananchi wangi katika maeneo yao.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela amewapongeza Wakuu wa Wilaya hao kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais ili waweze kusimamia wilaya hizo.
Aidha amewataka Wakuu wa Wilaya hao kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika utendaji kazi wao ikiwemo ya utoaji wa taarifa nje ya Mkoa.
“Ninawaomba mkawatumie vizuri wataalamu na vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo chini yetu kwa ajili ya kuwashauri na kuwapa utaalamu unaohitajika katika utekelezaji wa majukumu yenu” alisema Bwana Msovela.
Wakuu wa Wilaya walioapishwa leo ni Mheshimiwa Dkt. Vincent Mashinji kuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti; Mheshimiwa Juma Issa Chokoka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rorya; Mheshimiwa Joshua Samweli Nassari Mkuu wa Wilaya ya Bunda na Mwalimu Moses Rudovick Kaengele Mkuu wa Wilaya ya Buatiama.
Wengine ambao Mheshimiwa Rais amewahamishia katika Mkoa wa Mara ni Mhe. Dkt. Halfan Haule Mkuu wa Wilaya ya Musoma na Lt. Col. Michael Mangwela Mtenjele Mkuu wa Wilaya ya Tarime.
Shughuli ya uapisho huo umehudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samweli Kiboye, Viongozi wa Dini, Makatibu Tawala wa Wilaya, Meya wa Mji wa Musoma, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na watumishi , viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali na za binafsi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa