Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amewataka wakufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi, 2022 kuwafundisha na kuwa mfano mzuri kwa wasimamizi na makarani wa sensa katika Halmashauri zao ili kufanikisha zoezi la Sensa katika Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 26 Julai, 2022 wakati alipokuwa anafunga mafunzo ya sensa kwa wakufunzi wa sensa ngazi ya Mkoa yaliyofanyika katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare katika Manispaa ya Musoma.
“Serikali imetumia fedha nyingi kugharimia maandalizi ya Sensa hii, ninatambua pia kwa mwaka huu wengi wa makarani sio waajiriwa wa serikali, na hivyo ninaomba mkawafundishe kufanya kazi hii kwa uadilifu na kufuata miiko, taratibu na matakwa ya kazi hii” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha, Mheshimiwa Hapi amewaeleza wakufunzi hao kuwaelekeza wasimamizi na makarani wa sensa kuepuka masuala binafsi, tofauti za kisiasa, itikadi na kidini wakati wa kutekeleza zoezi la Sensa ili kuleta ufanisi wa zoezi hilo.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa sensa ni zoezi muhimu sana kwa Taifa kwa kuwa taarifa zitakazopatikana zitaisaidia serikali katika kupanga mipango ya maendeleo ya wananchi kwa kuzingatia mahitaji halisi.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amewataka waratibu wa Sensa kuhakikisha kuwa makarani wa sensa wanapata malipo yao kwa wakati ili kurahisisha utekelezaji wa shughuli za sensa kwa ufanisi.
“Ni vizuri makarani wote na wasimamizi na wahusika wengine wote kwenye zoezi la sensa wapate malipo yao kwa wakati ili kurahisisha utekelezaji wa zoezi la kukusanya taarifa kutoka kwa wananchi kwa ukamilifu” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha, amewaomba Waandishi wa Habari kuendelea kupeleka taarifa za sensa kwa wananchi ili wananchi waweze kupata taarifa sahihi na kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo tarehe 23 Julai, 2022.
Kwa upande wake, Mratibu wa Sensa Mkoa wa Mara Bwana David Danda ameeleza kuwa mafunzo ya wakufunzi wa sensa ngazi ya Mkoa yamefanyika kwa siku 21 kuanzia tarehe 6 Julai, 2022 na kuwahusisha wakufunzi 296 kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Bwana Danda ameeleza kuwa mpaka leo wakufunzi hao wamefundishwa, kufanya mitihani na kufuzu mafunzo yao na sasa wapo tayari kwa ajili ya kwenda kuwaelimisha wasimamizi na makarani wa sensa 69,000 ambao wamechaguliwa kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 inatarajiwa kufanyika hapa nchini tarehe 23 Agosti, 2022 na kuwahusisha watu wote watakaolala hapa nchini usiku wa kuamkia tarehe 23 Agosti, 2022.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa