Mkuu wa Mkoa wa Mara amelipongeza Kanisa la Waadventista Wasabato kwa kuwapa elimu ya UVIKO 19 waumini wao na kuwasistiza kuchanja Chanjo ya UVIKO 19 ili kupunguza makali ya ugonjwa huo.
Mheshimiwa Hapi ameeleza hayo leo tarehe 09 Oktoba 2021 katika eneo la Nyamongo Wilayani Tarime ambapo alikuwa mgeni rasmi katika kufunga mkutano na mahubiri ya AMANI ITOKAYO JUU yaliyokuwa yakirushwa moja kwa moja kwa waumini wa dhehebu hilo duniani kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ya kanisa hilo.
“Nimefurahi sana kusikia kuwa mlipokuwa hapa mmepata elimu juu ya UVIKO na chanjo ya UVIKO 19 na walioweza wamechanja, ninawapongeza sana” alisema Mheshimiwa hapi.
Amewahakikishia waumini wa dhehebu hilo kuwa chanjo ya UVIKO 19 ni salama na lengo la serikali kuileta nchini ni kupunguza athari za ugonjwa huo kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Hapi amelishukuru Kanisa hilo kwa kuisaidia serikali katika kutoa huduma za afya na elimu katika Mkoa wa Mara na maeneo mengine hapa nchini.
Mkuu wa Mkoa amelihakikishia Kanisa hilo ushirikiano kutoka kwa watendaji na viongozi wa serikali katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jimbo la Kaskazini mwa Tanzania Mchungaji David Makoye ameeleza kuwa katika Mkutano huo uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO 19 ulifanyika na waumini walipata huduma ya kuchanja kwa hiari baada ya kupewa elimu kuhusu chanjo ya UVIKO 19.
“Mkutano huu umesaidia sana waumini waliotaka kuchanjwa wamechanjwa hata ambao hawakutaka kuchanjwa wamepewa elimu kuhusu UVIKO 19 na umuhimu wa chanjo hiyo” alisema Mchungaji Makoye.
Mchungaji Makoye ameeleza kuwa katika mkutano huo huduma mbalimbali za afya zimetolewa ikiwa ni pamoja na uchunguzi na tiba ya afya ya kinywa na meno, macho, kugawa mewani, uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukizwa kama vile kisukari, shinikizo la dam una uzito uliokithiri.
Aidha alieleza kuwa katika mkutano huo elimu ya afya ya kinywa na meno ilitolewa kwa wanafunzi wa darasa la pili wa shule ya Msingi Kewanja na wanafunzi hao pia awaligawiwa dawa za meno na miswaki 300.
Mchungaji Makoye alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuja kufunga mkutano huo uliodumu kwa siku 21 ambao ulihusisha kanisa lote yaani majimbo Makuu mawili ya Kaskazini na Kusini mwa Tanzania la Kanisa la Waadventista Wasabato.
Ameeleza kuwa Jimbo la Mara lipo chini ya Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania na limeundwa na Mkoa mmoja wa Mara pamoja na Wilaya ya Ukerewe iliyopo katika Mkoa wa Mwanza na linajumla ya waumini 334,561 kwa sasa.
Mchungaji Makoye ameeleza kuwa Jimbo la Mara linaunga mkono juhudi za serikali kwa kutoa huduma katika sekta ya afya, elimu na huduma nyingine za kijamii.
Kwa upande wa Elimu jimbo la Mara linamiliki shule nane ambazo ni Shule ya Sekondari ya Ikizu, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Busegwe, Shule ya Sekondari ya Bwasi, Shule ya Seondari ya Nyansincha, Shule ya Sekondari ya Nyabohore na Shule ya Sekondari ya Kameya.
Mchungaji Makoye amezitaja shule nyingine kuwa ni Shule ya Msingi Murderspach pamoja na Hope International School.
Aidha ameeleza kuwa Jimbo la Mara linatoa huduma za afya kupitia zahanati 04 zinazomilikiwa na Kanisa hilo ambazo ni Zahanati ya Kamunyonge, Tarime, Bukwe na Nansio.
Mchungaji Makoye ameeleza kuwa katika mkutano huo, ulikuwa na vipindi mbalimbali ambavyo vilihusu masuala ya Watoto, ambacho kililongelea malezi kwa Watoto kiroho, kimwili, kiakili na kijamii; afya na familia ambacho kilizugumzia unyumba bora wenye mafanikio, kupunguza migogoro katika familia na jamii; afya kilizungumzia afya tiba, kinga, kutoa elimu dhidi ya mila na desturi zinazokinzana na maadili mema katika jamii.
Aidha kipindi cha neno la Mungu kilizungumzia malezi ya kiroho, kuwaandaa watu kuwa raia wema hapa duniani na katika ufalme ujao pamoja na kuombea amani Taifa letu na pia.
Mahubiri katika mkutano huo yametangazwa katika eneo la Nyamongo, kitaifa na kimataifa kupitia televisheni, radio na mitandao ya kijamii ya kanisa hilo baada ya kutafsiriwa katika lunga za Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kireno na lugha ya alama kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum.
Katika msafara wake Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samweli Kiboye (Namba 3) na Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtengele.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa