Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amewapongeza wananchi wa eneo la Kirumi katika wilaya ya Butiama kwa kuanzisha ujenzi wa Zahabati ya Kirumi ambayo sasa serikali imeongeza fedha za kupanua kuwa Kituo cha Afya.
Mheshimiwa Hapi ametoa pongezi hizo leo tarehe 8 Oktoba, 2021 katika eneo hilo baada ya kugagua maendeleo ya ujenzi na kupatiwa taarifa ya maendeleo ya mradi huo.
“Mimi niwapongeze sana kwa jitihada zenu za kubuni na kuanzisha mradi huu ambao sasa serikali unaenda kuupanua ili huduma zote muhimu ziweze kupatikana hapa” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amemwagiza Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuwa katika jengo la awali, chumba cha kujifungulia na wodi ya waliojifungua viongezwe ukubwa ili kukidhi mahitaji.
MKuu wa Mkoa pia amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Butiama kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi hiyo ili kuendana na matamanio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika mradi huo.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa fedha iliyoletwa Kirumi ni sehemu ya shilingi 1,550,000,000 zilizoletwa katika Mkoa wa Mara kwa ajili ya kujenga vituo vya afya katika Wilaya ya Serengeti, Butiama, Rorya, Bunda na Tarime.
Ameeleza kuwa Wilaya ya Butiama imepata bahati ya kupata vituo viwili ambapo kuna Kituo cha Kirumi kilichopata milioni 300 na Kituo cha Afya Makongoro kilichopata milioni 250 katika mgao huo.
Mheshimiwa Hapi amewataka wahusika wa mradi huo kuusimamia vizuri ili uweze kuleta matokeo yanayotarajiwa na serikali ya awamu ya sita.
“Ninawapongeza sana kwa kuanza kujenga shule ya msingi mpya katika eneo hili ambayo itawasaidia Watoto kupata elimu karibu na mazingira yao, Mkurugenzi fuatilia maendeleo ya ujenzi na halmashauri ikamilishe ujenzi wa shule hiyo na isajiriwe” alisema Mheshimiwa Hapi.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji wa Kijiji cha Kirumi Bi. Vailet Francis Kisumo ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwaka 2010 kwa nguvu za wananchi.
“Halmashauri ya Wilaya ya Butiama iliongeza shilingi milioni 128 kwa nyakati tofauti ili kuweza kukamilisha jengo hilo” alisema Bi. Kisumo.
Bi, Kisumo ameeleza kuwa kwa sasa Kijiji cha Kirumi kimepokea shilingi milioni 300 kutoka serikalini kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo pamoja na kujenga kichomea taka na maabara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa