Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ushirikiano, utulivu, uzalendo na mshikamano walioionyesha wakati wote ambapo Mkoa ulipata ugeni mkubwa wa viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali walioshiriki katika maadhimisho ya miaka 45 ya CCM na ziara ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya miradi ya maendeleo kilichofanyika leo tarehe 15 Februari 20222 katika ukumbi wa uwekezaji uliopo katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Hapi amesema wananchi walionyesha uzalendo wa hali ya juu.
“Wananchi walihakikisha kuwa ziara ya Mheshimiwa Rais inafanyika kwa amani, utulivu na hamasa kubwa sana, kwa niaba ya viongozi wote wa Mkoa wa Mara ninawapongeza sana” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amewataka wananchi kuendelea na uzalendo huo kwa manufaa ya wananchi wenyewe lakini na taifa kwa ujumla.
Aidha amevipongeza vyombo vya usalama kwa kusimamia amani na utulivu katika maeneo yote ya Mkoa wa Mara na kuhakikisha wageni wote wanarudi majumbani kwao wakiwa salama.
Mheshimiwa Hapi pia amewashukuru wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara ambao walitoa huduma mbalimbali kwa wageni waliokuja na kuujengea sifa Mkoa wa Mara.
“Wafanyabiashara wengi waliitikia wito wa kufanya biashara zao saa 24 kwa siku ambazo wageni walikuwepo katika Mkoa wa Mara, hii ilisaidia kutoa huduma kwa wageni ambao walichelewa kufika na ambao walihitaji kuamka mapema kuwahi sehemu mbalimbali.
Aidha, Mheshimiwa Hapi amewataka wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara kuendelea kuboresha huduma katika biashara zao kwa kuwa wageni wameondoka na sifa nzuri za Mkoa wa Mara wengine watapenda kuja tena wakati mwingine wakute huduma bora zaidi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kujitokeza kwa wananchi kwenye mikutano na maeneo ambayo Mheshimiwa Rais alikuwa anapita ni ishara nzuri kuwa wananchi wengi wanaipenda serikali yao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara ya siku nne katika Mkoa wa Mara ambapo alikuwa Mgeni Rasmi wa Maadhimisho ya miaka 45 ya Uhuru, aliweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Mgango- Kiabakari- Butiama, alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa) na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji Bunda.
Aidha katika ziara hiyo Mheshimiwa Rais alizungumza na wananchi katika Uwanja wa Karume uliopo Manispaa ya Musoma, eneo la Mgango, Kwangwa, Butiama na Mji wa Bunda.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Rais pia alitembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika eneo la Mwitongo ambapo pamoja na mambo mengine alizuru na kuweka Shada la Maua katika kaburi la Baba wa Taifa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa