Mkuu wa Mkoa wa Mara leo amewaongoza wananchi wa Wilaya ya Musoma kupanda miti 1,000 katika Shule ya Sekondari ya Kiara kama sehemu ya Maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Akizungumza baada ya zoezi la upandaji miti, Mheshimiwa Hapi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kupanda miti ili kulinda mazingira ya Mkoa wa Mara kwa ajili ya vizazi vijavyo.
“Miti hii ambayo kivuli chake tunakipata leo, ilipandwa na wazee wetu hapo zamani na sasa ni wajibu wetu kupanda miti na kutunza mazingira” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amewataka wanafunzi na walimu wa shule zote za Mkoa wa Mara kupanda miti katika maeneo yao ili kulinda uoto wa asili wa Mkoa wa Mara.
Akitoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa, Meya wa Manispaa ya Musoma Mheshimiwa William Gumbo ameeleza kuwa Shule ya Sekondari ya Kiara imechaguliwa kuzindua zoezi la upandaji miti kutokana na sababu za kihistoria.
“Serikali ilipoanza kujenga shule za kata, shule ya kwanza kujengwa na wananchi wa Manispaa ya Musoma ilikuwa ni Sekondari ya Kiara, mwitikio ulikuwa mkubwa sana na nguvu za wananchi zilifanikisha ujenzi wa shule nzima ndani ya muda mfupi” alisema Mheshimiwa Gumbo.
Mheshimiwa Gumbo ameeleza kuwa hata zoezi hili la upandaji wa miti linaweza kufanikiwa sana kutoakana na uzoefu huo na mwitikio wa wananchi katika ujenzi wa Shule hiyo.
Mstahiki Meya amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuungana na wananchi wa Manispaa ya Musoma kupanda miti kama sehemu ya uzinduzi wa kampeni ya kupanda miti 30,000 katika Manispaa ya Musoma.
Mheshimiwa Gumbo ameeleza kuwa zoezi la kupanda miti katika Manispaa ya Musoma ni endelevu na kuwataka wanafunzi na wananchi kuchukua miche ya miti katika kitalu cha Wakala wa Misitu (TFS) Manispaa ya Musoma na kupanda katika maeneo yao.
Zoezi la kupanda miti lilihudhuriwa pia na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, wakuu wa taasisi za serikali na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Wengine waliohudhuria ni Meya wa Manispaa ya Musoma, Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Wakuu wa Idara na Vitengo vya Manispaa ya Musoma na watumishi wa Manispaa ya Musoma, wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari ya Kiara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa