HAPI ATOA WIKI MBILI KWA VETA KUKAMILISHA KAZI
Mkuu Wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amekitaka Chuo cha VETA Mara kukamilisha kazi ya kutengeneza nguzo za majina ya barabara waliyopewa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Mara.
Akizungumza wakati wa kukagua na kujionea utengenezaji wa nguzo hizo, Mheshimiwa Hapi ameridhishwa na ubora wa kazi inayofanywa na Chuo cha VETA Mara na kuwataka kukamilisha kazi hiyo ndani ya wiki mbili.
“Nataka hii kazi iwe imekamilika ndani ya wiki mbili hadi tarehe 19 Juni, 2022 kazi hii iwe imekamilika na nitakuja kukagua kuona kazi ilivyofanyika” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha Mheshimiwa Hapi amekitaka Chuo hicho kuongeza mafundi zaidi katika zoezi la kupaka rangi na kuandika majina ya barabara ili kazi hiyo iweze kukamilika kwa haraka.
“Mkiona inafaa mnaweza kuwatumia wanafunzi wa Sekondari ya Ufundi Musoma wanaosomea masuala ya rangi wakawasaidia na ikawa kama sehemu yao ya mafunzo kwa vitendo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kuwahamasisha wananchi kuweka nguzo na majina ya mitaa yao ili iweze kutambulika kwa urahisi.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA Mkoa wa Mara Mhandisi Boniface William ameeleza kuwa TARURA imewapa VETA kazi ya kutengeneza nguzo 5892 za barabara za TARURA kwa gharama ya shilingi milioni 206.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Mhandisi William ameeleza kuwa vifaa vya mradi huo vimenunuliwa na TARURA kwa gharama ya shilingi zaidi ya milioni 500.
“Hii kazi imeletwa VETA kwa sababu tuliamini VETA wataifanya kwa ubora na viwango vinavyotakiwa katika kufanikisha operesheni hii ya anuani za makazi” alisema Mhandisi William.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Mara Mwalimu David Louis ameeleza kuwa kwa mujibu wa mkataba kazi hiyo ilitolewa tarehe 13 Mei, 2022 na ilipaswa kukamilika tarehe 13 Juni, 2022.
“Kwa sasa kazi ya ukataji wa mabomba na utengenezaji wa vibao imekamilika na kazi ya kupaka rangi na kuandika majina imeanza na inaendelea” alisema Mwalimu Louis
Mwalimu Louis ameeleza kuwa katika kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wataongeza mafundi na vibarua ili kuharakisha zoezi hilo.
Utengenezaji wa nguzo za majina ya barabara ni sehemu ya utekelezaji wa Operesheni ya Anuani za Makazi ambayo imefanyika hapa nchini na kufikia mwisho tarehe 30 Mei, 2022.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa