Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amemtaka mkandarasi wa mradi wa barabara ya Butiama- Makutano kulipa deni Service Levy analodaiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ndani ya wiki mbili.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo hayo wakati leo tarehe 19 Julai 2021 alipokuwa katika ziara ya siku moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama katika mradi wa barabara wa Butiama- Makutano.
“Nenda ukalipe pesa zetu shilingi zaidi ya milioni 80 ndani ya wiki mbili ili halmashauri iende kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi” amesema Mheshimiwa Hapi.
Aidha amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara kuhakikisha mkandarasi anafanyakazi kwa haraka kukamilisha barabara hiyo ambayo inaingia eneo la Butiama hadi nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na maeneo mengine katika Wilaya ya Butiama.
Katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara amepiga marufuku mkandarasi kutumia kokoto, kifusi na mchanga wa kujengea kutoka mikoa mingine na kuamuru atumie zinazotoka katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Butiama Mheshimiwa Jumanne Sagini ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umechukua muda mrefu sana, barabara hii ina urefu wa kilometa 50 lakini ujenzi wake umechukua muda wa zaidi ya miaka sita mpaka sasa.
“Jambo hili linawakera wananchi kwa sababu barabara nyingine za urefu huu zinakamilika wakati hii inakuwa inaendelea kujengwa bila sababu za msingi” alisema Mheshimiwa Sagini.
Ameeleza kuwa wananchi wa Butiama walikuwa wamesikitika sana baada ya mkandarasi kuleta kokoto na malighafi za kujengea barabara hiyo kutoka Mkoa wa Geita, na kuwa anashukuru jambo hilo kwa sasa mkandarasi amelirekebisha.
“Tunafurahi kama ameanza kuchimba kokoto hapa kwa sababu kwanza ataipatia halmashauri yetu mapato lakini pili vijana wetu watajipatia ajira kwenye maeneo haya” ameeleza Mheshimiwa Sagini.
Mheshimiwa Sagini ameeleza kuwa vipande vya barabara vilivyobakia kati ya Butiama na Makutano ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Butiama kwani inasababisha barabara hii ionekane haiishi kwa muda mrefu sana.
Aidha Mheshimiwa Sagini ameeleza kuwa wananchi pia wanalalamikia suala la ulipaji wa fidia kwa baadhi ya nyumba zilizokuwepo katika eneo la barabara na malipo yao yapo na wananchi ambao hawajachukua fidia zao waende wakachukue kwenye ofisi za TANROADS Mkoa wa Mara.
Akitoa maelezo ya mradi huo, Mshauri Mwelekezi katika mradi huo ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulianza rasmi mwaka 2013 na wakati unaanza kulikuwa na vitu vingi ambavyo vilikuwa havijakaa sawa na hivyo kusababisha changamoto katika utekelezaji wa mradi huo.
“Mshauri Mwelekezi alikuwa hajapatikana na ilichukua takriban miezi sita kumpata na baadaye alipokuja lilijitokeza tatizo kuwa mradi haukuwa sawasawa, Mshauri mwelekezi alilifanyiakazi na ilichukua muda mrefu baadaye kufanyia kazi changamoto mbalimbali za mradi kabla ya mradi kuanza kutekelezwa” alisema Mshauri Mwelekezi.
Mshauri Mwelekezi ameeleza kuwa kwa sasa mradi umekuwa unakwama kutokana na mkandarasi JV constructions Limited kutegemea fedha anayolipwa ndio aendelee na kazi na malipo yakikwama na kazi inakwama. Mshauri Mwelekezi ameeleza kuwa kwa sasa mkandarasi amelipwa kiasi cha bilioni 1.7 na kazi imeanza tena kutekelezwa.
Mshauri Mwelekezi ameeleza kuwa kwa sasa mradi huo ambao unatengenezwa kwa gharama ya bilioni 60 unatarajiwa kukamilika tarehe 15 Desemba 2021 na mpaka sasa kazi hiyo imekamilika kwa asilimia 89.
Ameeleza kuwa ujenzi wa madaraja yote ya mradi huo yamekamilika kilichobakia ni vipande vya barabara ambavyo bado hajakamilisha kulingana na michoro na makubaliano ya mkataba.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Butiama, viongozi wa taasisi za serikali na viongozi wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa