Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameiagiza Sekretariati ya Mkoa wa Mara kukamilisha miradi mine ya ujenzi na ukarabati wa nyumba za viongozi wa huu inayotekelezwa katika Manispaa ya Musoma.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo hayo leo tarehe 14 Julai 2021 katika ziara yake aliyoifanya kukagua miradi mine inayotelekelezwa kwa mfumo wa force account na kusimamiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara katika Manispaa ya Musoma.
“Ninatoa wiki mbili miradi hii minne yote iwe imekamilika…..ninataka ofisi yangu iwe ni ofisi ya mfano katika utekelezaji wa miradi ya serikali katika Mkoa wa Mara” alisema Mheshimiwa Hapi.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi, usimamizi na ugawaji wa kazi kwa mafundi wa miradi hiyo ambao wanaajiri mafundi wengine katika utekelezaji na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha Mkuu wa Mkoa ameagiza kupatiwa taarifa ya kina kuhusu matumizi ya fedha na hususan fedha zilizotumika katika manunuzi ya vifaa na kulipa mafundi katika miradi hiyo.
Awali akitoa taarifa ya miradi hiyo Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Miundombinu Mhandisi Faustin Tarai ameeleza kuwa miradi hiyo ilianza kutekelezwa kuanzia tarehe 15 Machi 2021 na inatarajiwa kukamilika tarehe 19 Julai 2021.
Aidha Bwana Tarai ameeleza kuwa kuwa vifaa vyote kwa ajili ya miradi hiyo vilishanunuliwa na malipo ya mafundi yanaendelea kutolewa kulingana na madai wanayoyatoa baada ya kukamilisha sehemu ya kazi.
Katika kukagua miradi hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela; Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mheshimiwa Alfany Haule, Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Sekretariati ya Mkoa, wataalamu wa ofisi ya Katibu Tawala Wilaya ya Musoma pamoja na waandishi wa habari.
Miradi inayotekelezwa na Sekretariati ya Mkoa wa Mara katika Manispaa ya Musoma ni pamoja na ujenzi wa nyumba ya Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya; ujenzi wa nyumba ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma; ukarabati wa nyumba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara; na ukarabati wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Musoma ambayo imefikia katika hatua tofauti za ukamilishaji wake.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa