Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amewataka wathamini kutoka katika ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali kukamilisha zoezi la uthamini wa ardhi katika eneo la Komelera ndani ya siku 20.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 12 Agosti 2021 wakati alipotembelea eneo hilo kujionea kazi ya tathmini ya maeneo ya wananchi yanayotarajiwa kuchukuliwa kwa ajili ya upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
“Haiwezekani ninyi mnauwezo wa kufanya uthamini wa ekari 50 kwa siku moja lakini kazi mnayofanya sasa ni ekari tano kwa siku jambo ambalo linachelewesha uthamini huu kukamilika.
Mheshimiwa Hapi amewaagiza viongozi na watendaji wa Wilaya ya Tarime kutoa ushirikiano kwa wathamini hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na haraka.
Aidha amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Tarime/Rorya kuongeza ulinzi katika eneo la tathmini ili kuondoa vurugu yoyote wakati wa zoezi la tathmini katika eneo hilo.
Mheshimiwa Hapi amewaonya wananchi watakaofanya vurugu katika eneo hilo na kuchelewesha uthamini kuwa hawatavumiliwa kuvuruga zoezi hilo sheria itachukua mkondo wake.
Mheshimiwa ametoa tahadhari kuwa mwekezaji akiona anacheleweshwa kuendelea na mradi wake anaweza kutaka kuhamishia mgodi wake sehemu ambayo haina vurugu kama za Tarime maana maeneo yenye dhahabu yapo mengi hapa nchini.
Amewataka Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Vijiji kusimamia uthamini huo ili kutatua migogoro inayojitokeza ili wathamini waendelee na uthamini bila kubuguziwa na mtu yoyote.
Kwa upande wake Mthamini kutoka Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali Bwana Rashid Magetta ameeleza kuwa kwa sasa uthamini unafanywa na wataalamu 54 hata hivyo kazi hiyo haiendi kwa kasi inayotakiwa kutokana na changamoto mbalimbali.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na wananchi kuendelea kupanda mazao wakati huu wa uthamini katika maeneo ambayo yanaendelea kuthaminishwa; migogoro ya wananchi kugombea ardhi; wananchi kuendelea kuuziana ardhi wakati huu wa uthamini na migogoro ya mipaka ya vijiji baina ya viongozi wa vijiji.
Amezitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya maeneo kuwa na hati na kuvamiwa na wavamizi ambao nao wanataka wathaminiwe wakati maeneo sio yakwao kiuhalali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa