Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ametoa mwezi mmoja Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya akamilishe ujenzi wa choo katika Shule ya Sekondari ya Buturi iliyopo katika Mji wa Shirati.
Akizungumza katika mkutano wa wananchi katika Mji wa Shirati leo tarehe 15 Julai 2021 Mheshimiwa Hapi amepokea malalamiko kutoka kwa mwananchi kuhusu shida ya vyoo inayowakabili wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Buturi.
“Ninatoa mwezi mmoja hadi tarehe 15 Agosti 2021 choo cha Sekondari ya Buturi kiwe kimekamilika na kinahudumia wanafunzi wa shule hiyo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha Mheshimiwa Hapi ameagiza kuacha mara moja kutoza shilingi 2,000 kwa wafanyabiashara wa chakula kwa ajili ya fomu ya kupima afya na badala wake wafanyabiashara wapatiwe fomu hiyo wakatoe nakala.
Mkuu wa Mkoa wa Mara alitoa maagizo hayo kufuatia Bwana Musa Mbogo kueleza kero ya choo katika Sekondari ya Katuru na jitihada ambazo wananchi walizifanya kunusuru hali hiyo.
Bwana Mbogo ameeleza kuwa baada ya wananchi kuona wanafunzi wa shule hiyo hawana choo walichangia kuchimba shimo, matofali na fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa choo hicho lakini fedha hizo kiongozi mmoja wa mtaa aliyehusika katika kuzikusanya amekimbia nazo.
Aidha Bwana Mbogo ameeleza kero nyingine kuwa ni zahanati ya eneo hilo ambayo ilikuwa inajengwa kwa nguvu za wananchi ambayo imesimama kwa muda mrefu bila taarifa za kueleweka.
Akitoa majibu ya kero hiyo Mtendaji wa Kata hiyo alieleza kuwa ni kweli wanachi walichangia nguvukazi, matofali na fedha kujenga choo na mhusika ametoroka na fedha hizo na kwa sasa kesi imelipotiwa polisi na mtuhumiwa bado anaendelea kutafutwa.
Aidha Mtendaji wa Kata alieleza kuwa kwa sasa walimueleza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Rorya ambaye aliahidi kutoa fedha kukamilisha ujenzi wa choo hicho.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ameeleza kuwa alipewa taarifa na watendaji, alitenga shilingi milioni 3 ambazo zitakuja kukamilisha Chuo hicho.
Aidha katika mipango ya muda mrefu Halmashauri kwa kutumia bajeti ya 2021/2022 imetenga milioni 25 kutoka mradi wa P4R kwa ajili ya kujenga vyoo vingine katika Shule ya Sekondari ya Buturi.
Aidha Mkurugenzi aliahidi kufuatilia fedha shilingi 2,000 ambayo ilikuwa inatozwa na Afisa Afya kwa wafanyabiashara wa chakula kama ilikuwa inaingia kwenye mfuko wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Katika mkutano na wananchi uliofanyika katika Mji wa Shirati, Mkuu wa Mkoa alitoa nafasi kwa wananchi kueleza kero zao na kuuliza maswali ambayo yalikuwa yanajibiwa na waatendaji mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Mkuu wa Mkoa wa Mara alifanyaziara ya siku moja katika Wilaya ya Rorya na Tarime kukagua miradi ya Maji na mpaka wa Tanzania na Kenya katika wilaya hizo na aliongea na wananchi katika maeneo mbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa