Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi katika Mkoa wa Mara kuwajibika kwa mujibu wa mikataba yao na kukamilisha miradi kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma.
Akizungumza katika kikao na wakandarasi wote wanaotekeleza miradi katika Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Hapi amewakumbusha wakandarasi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mikataba yao bila kusukumwa na wasimamizi wa miradi hiyo.
“Haiwezekani mkandarasi umeomba kazi, umepewa, sasa kutekeleza hadi uitwe na polisi na usimamiwe ili utekeleze mradi ulioomba wewe mwenyewe, hiyo haikubaliki” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ametoa mwezi mmoja kwa wakandarasi wa miradi ya barabara zinazosimamiwa na TARURA na TANROADS wanaolalamikiwa kuchelewesha miradi kuikamilisha miradi hiyo.
Mheshimiwa Hapi amewataka wasimamizi wa wakandarasi na wakandarasi wote kuheshimu mamlaka za serikali katika ngazi za Mkoa, Wilaya ya Halmashauri wanazofanyiakazi na kutoa ushirikiano kwa viongozi wa mamlaka hizo katika kutekeleza miradi ya waanchi.
Aidha Mheshimiwa Hapi amewataka Wakuu wa Wilaya kusimamia na kuhakikisha wanapata taarifa za miradi yote inayotekelezwa na mamlaka mbalimbali katika maeneo yao.
“Wakuu wa Wilaya msikubali taasisi na wakandarasi waende kukabidhiana miradi gizani bila ya uwepo wa wananchi na viongozi katika makabidhiano ya miradi hiyo, daini taarifa” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amewataka wakandarasi wote kulipa ushuru wa huduma (service levy) kwa Halmashauri kutokana na kazi wanazozifanya katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Bwana Langaeli Akiyoo ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameleta fedha nyingi za kutekeleza miradi katika Mkoa wa Mara lakini miradi hiyo mingi haitekelezwi vizuri.
“Tulipita kukagua miradi ya maendeleo, miradi mingi ipo chini ya kiwango au utekelezaji hauendani na michoro ya awali (BOQ) ya mradi husika hususan miradi ya barabara” alisema Bwana Akiyoo.
Aidha Bwana Akiyoo amewataka wakandarasi kufanyakazi kwa ushirikiano na viongozi waliopo katika maeneo miradi inapotekelezwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakandarasi wa Mkoa wa Mara Mhandisi Municali Mseti amewataka wakandarasi kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma kwa weredi na kwa wakati.
“Ukandarasi ni biashara ya kitaaluma, ambayo kutoifanya vizuri kunaidhalilisha taaluma hii ya uhandisi ambayo wengi wetu tumeisomea na tunaifanyia kazi” alisema Bwana Mseti.
Aidha Bwana Mseti ameiomba serikali kuwalipa wakandarasi kwa wakati pale wanaokuwa wanadai baada ya kufanyakazi zao.
Kabla ya kufunga kikao hicho wakandarasi wote wamekula kiapo cha kutekeleza majukumu yao vizuri na kutii mamlaka za Serikali zilizopo katika maeneo wanapotekeleza mradi yao.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Meya na Wenyeviti wa Halmashauri, wakuu wa taasisi, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wandandarasi na wakandarasi wenyewe.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa