Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuchukua hatua za maksudi kuboresha utekelezaji wa afua za Lishe ili kuboresha lishe ya wananchi wa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo hayo wakati wa kikao cha tathmini ya masuala ya lishe kilichofanyika leo katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Haiwezekani kadi alama ya lishe kwa kipindi cha nusu mwaka bado inaonyesha Mkoa wa Mara tupo kwenye alama nyekundu katika kutoa fedha na katika kuweka katika bajeti fedha inayohitajika kwa kila mtoto wa chini ya umri wa miaka mitano” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuwachukulia hatua Maafisa Lishe na watendaji wengine wote wanaokwamisha utekelezaji wa afua za lishe katika Mkoa wa Mara.
“Kila mtu awasimamie watu wa eneo lake na wakichukuliwa hatua ushahidi ubaki katika mafaili yao ili kuhakikisha kuwa kazi zinafanyika kwa ufanisi, weredi na uzalendo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameagiza vikao vya tathmini ya masuala ya lishe kufanyika katika ngazi za Halmashauri na Wilaya mwishoni mwa mwezi Machi, 2022 ili mapungufu yanayoonekana yafanyiwe kazi kabla ya kuletwa katika kikao cha tathmini ya lishe kwa ngazi ya Mkoa.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuangalia uwezekano wa kuingiza fedha za miradi ya wadau wa maendeleo katika bajeti zake ili ziweze kutumika pamoja na mambo mengine kutekeleza masuala ya afua za lishe.
Awali, taarifa ya utekelezaji wa afua za lishe, Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2021 hadi Desemba, 2021 zilitenga fedha chini ya asilimia 50 inayohitajika lakini hata kiasi hicho cha fedha kilichotengwa pia kilitumika kwa kiasi kidogo au hakikutumika kabisa katika kipindi hicho.
Aidha, katika taarifa hiyo, Halmashauri nne hazikutenga pesa wala hazikutumia pesa kabisa katika kipindi hicho cha tathmini, Halmashauri hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Mnispaa ya Musoma, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Wakitoa maelezo kuhusiana na hali hiyo, wakurugenzi wa Halmashauri zote wamekiri kutenga na kutumia fedha ambazo zilitokana na wadau wa maendeleo na fedha za mapato ya ndani lakini hazikuonekana kwenye mfumo wa lishe kutokana na kuwa hazikuingizwa kwenye bajeti ya Halmashauri au zilitumika baada ya tarehe 15 Desemba, 2021 na hivyo kutoonekana katika tathmini ya wakati huu badala yake zitaonekana katika kipindi kijacho cha tathmini.
Kikao cha tathmini ya afua za lishe katika Mkoa wa Mara kimehudhuliwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Bwana Benjamini Oganga, Wakuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Idara za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Halmashauri na Maafisa Lishe wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa