Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amemuagiza mkandarasi wa mradi wa maji wa Mgango-Kiabakari kuhakikisha anaajiri vibarua katika ujenzi wa mradi huo kutokana na wananchi wa Mkoa wa Mara na kununua baadhi ya vifaa ya ujenzi huo kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara ili kuleta maendeleo ya Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo hayo leo tarehe 19 Julai 2021 wakati akikagua mradi wa maji wa Mgango- Kiabakari na kujionea ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya upanuzi wa mradi huounaosambaza maji katika sehemu kubwa ya vijiji vya Wilaya ya Butiama.
“Tunataka fedha ya mradi huu inawanufaishe wananchi wa Mkoa wa Mara na baadaye hawa ndio watakaotusaidia katika ulinzi wa miundombinu ya mradi huu” alisema mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amemuagiza mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo hususan eneo linapojengwa miundombinu ya kuchuja maji jirani na chanzo cha maji kwani mvua zikianza kazi haitaweza kuendelea.
“Hapa ninataka kazi ifanyike usiku na mchana na vibarua waongezwe ili kasi ya ujenzi iongezeke, mvua zikianza zikute mradi huu umeshakaa sawa na uweze kuendelea hata kipindi cha mvua” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji ya Mgango- Kiabakari kufanya mchakato wa haraka kununua pampu na kumtafuta mkandarasi wa kuifunga pampu hiyo ili huduma ya maji iweze kurejea katika wilaya ya Butiama kufuatia kuungua kwa pampu iliyokuwa inasukuma maji katika mradi wa zamani.
Aidha amewataka wananchi wanaotegemea maji kutoka katika Mamlaka ya Mgango- Kiabakari kuwa na subira katika kipindi hiki ambapo mchakato wa kununua pampu mpya unaendelea ili kuweza kufuata sheria za manunuzi.
Awali akitoa taarifa ya Mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji ya Mgango- Kiabakari Mhandishi Cosmas Sanda ameeleza kuwa Mamlaka hiyo kwa sasa inamiradi miwili mradi mpya ulioanza kujengwa na mradi wa wazamani na yote haitoi maji kwa wananchi.
“Mradi wa zamani hautoi maji kwa sababu pampu ya kusukuma maji imekufa lakini tayari serikali imetoa fedha na mchakato wa manunuzi ya kununua pampu na mtaalamu wa kufunga pampu hiyo unaendelea, tunategemea wananchi wataanza kupata maji baada ya miezi miwili” alisema Mhandisi Sanda.
Aidha Mhandisi Sanda ameeleza kuwa mradi wa pili ujenzi wake mkandarasi wake alipatikana tarehe 17 Desemba 2020 na mradi ulianza kujengwa Machi 2021 baada ya Government Notice kutolewa na mradi huo unategemewa kutekelezwa kwa miezi nane kwa gharama ya shilingi bilioni 70.78.
“Kwa sasa mradi huu mpya upo umekamilika kwa asilimia 14 jumla katika kazi zinazohusisha ujenzi wa matanki ya maji, kusambaza mabomba, kukarabati baadhi ya matanki ya mradi wa zamani, kujenga nyumba ya watumishi na chujio la kusafishia maji na nyumba ya mtumishi” alisema Mhandisi Sanda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa