Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kuwa na mkakati ambao utaisaidia halmashauri hiyo kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 14 Agosti 2021 wakati alipokuwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
“Mkakati wa mapato ya halmashauri uuangaliwe upya ili kuona kama kuna vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha ukusanyaji katika vyanzo vya zamani” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha ameitaka Halmashauri kukusanya kikamilifu kutoka kwenye vyanzo vyote vya mapato vya halmashauri ili kuweza kuboresha huduma za jamii katika halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Hapi ameitaka Halmashauri pia kuwekeza kwenye baadhi ya shughuli za wananchi kama vile kilimo au biashara ambavyo vinategemea kuleta mapato ya halmashauri hapo baadaye.
“Mnaweza kuamua kusimamia wananchi wapate ushauri wa kulima mazao ya biashara au chakula ambayo mnajua wakipata kwa wingi yakiuzwa, halmashauri itapata mapato kutokana na kilimo hicho” alisema Mheshimiwa Hapi.
Ameishauri Halmashauri kuwashirikisha watendaji wa Kata na Vijiji pamoja na Maafisa Tarafa katika zoezi la kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kuona uwezekano wa kupanua zaidi uwigo wa vyanzo hivyo na kupokea ushauri wa watendaji hao katika ukusanyaji wa mapato.
Mheshimiwa Hapi amesistiza usimamizi wa matumizi wa mashine za kukusanyia mapato (POSS) zifanyekazi muda wote na mapato yakishakusanywa yaende benki yasitumike kabla ya kuingizwa benki.
Aidha ameitaka Halmashauri hiyo kudhibiti matumizi ya fedha za serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi moja kwa moja.
Mheshimiwa Hapi amewataka watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa kusimamia usomaji wa mapato na matumizi ya vijiji kwa wananchi wa vijiji husika ili kupunguza malalamiko ya wananchi kwa serikali yao.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mheshimiwa Juma Chikoka ameeleza kuwa katika Wilaya ya Rorya anavyovipaunmbele ambavyo atavisimamia kwa juhudi na maarifa.
Mheshimiwa Chikoka amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja kuimarisha ukusanyanji wa mapato ya Halmashauri ya Rorya kwa kulinda vyanzo vya mapato vilivyopo na kubuni vyanzo vipya vya mapato.
“Ninauhakika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri ukiimarishwa, mambo mengine mengi yatakuwa rahisi kufanikiwa hivyo kuongeza huduma za jamii kwa wananchi wa Wilaya ya Rorya” alisema Mheshimiwa Chikoka.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Hapi alikagua miradi ya maendeleo, kuzungumza na wananchi na kuzungumza na viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa