HAPI ATAKA MAELEZO UJENZI WA CHOO KITUO CHA AFYA CHANGUGE
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya Bwana Charles Chacha Marwa na timu yake kutoa maelezo ya matumizi ya shilingi milioni 22 kujenga choo katika Kituo cha Afya cha Changuge kilichopo katika Halmashauri hiyo.
Mheshimiwa hapi ametoa maagizo hayo leo tarehe 23 Julai 2021 wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara ilipotembelea na kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM katika halmashauri hiyo.
“Haiwezekani choo hiki chenye matundu sita kutumia milioni 22 wakati sehemu nyingine tunajenga tundu moja la choo kwa shilingi milioni 1,100,000 tu lakini hapa fedha hii ni kubwa sana na sisi hatujaridhika na kazi hii” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amemtaka Mkurugenzi kuambatana na wahusika wote katika mradi huo na kuwasilisha maelezo yao kesho tarehe 24 Julai 2021 saa nne kamili.
“Mje na mambo mawili, maelezo au fedha zilizobakia katika maradi huo…..nikiona jinai nitatoa maagizo kwa Jeshi la Polisi liwaweke ndani na kupelekwa mahakamani” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kumpangia majukumu mengine Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho Dkt. Respicous Rugemalila na kuondoa uongozi wote wa kituo hicho baada ya kukuta mazingira machafu katika kituo hicho.
“Chama na Serikali hatujaridhika na mazingira ya kituo hiki, ni pachafu na hii sio sawa kabisa, huwezi kuwa na kituo cha afya kichafu namna hii halafu watu wamekaa tu hapa” alisema Mheshimiwa Hapi.
Ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kuhakikisha kuwa anaunganisha mfumo wa mapato ya serikali (GOTHOMIS) katika kituo hicho ili kudhibiti mapato ya serikali.
Mkuu wa Mkoa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kuwasismamisha kazi watumishi ambao walikuwa zamu zamu wakati vifaa vinaibiwa na kuwafungulia mashauri ya kiutumishi kulingana na makosa yao kiutumishi na kuhakikisha kuwa vifaa vinapatikana na visipo patikana wakatwe mishahara yao kufidia hasara hiyo.
Mheshimiwa Hapi amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi Utegi kuchunguza upya wizi wa vifaa katika kituo hicho unaorudia rudia mara kwa mara.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samweli Kiboye ameeleza kuwa chama kimepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na Kituo cha Afya Chenguge.
Ameeleza kuwa Chama cha Mapinduzi hakijaridhishwa na matumizi ya fedha hiyo yote katika mradi huo wa Choo.
“Hii hospitali ni ya siku nyingi sana na CCM tumepiga kelele sana, tunashukuru sana kwa hatua ulizozichukua leo na Chama kipo nyuma yako, na Chama hakijaukubali mradi huu” Mheshimiwa Kiboye.
Mheshimiwa Kiboye ameeleza kuwa Kituo hicho ni kichafu sana na hakina maji ya uhakika na wagonjwa wanakuja na maji yao.
Aidha Mheshimiwa Kiboye ameeleza kuwa kuna vifaa vya maabara vimeibiwa tarehe 8 Machi 2021 katika hospitali hiyo na kuongeza kuwa kituo hicho kimekuwa kikiibiwa vifaa mara kwa mara na wizi wa mwezi Machi ni mara ya sita tangia uanze wizi huo.
Kamati ya siasa katika Wilaya ya Rorya ilitembelea pia mradai wa vijana wa bodaboda, Shule ya Sekondari Nyanduga, mradi wa ujenzi wa barabara, Hospitali ya Wilaya ya Rorya na Kituo cha Afya Changuge.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa