Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amewataka viongozi, watendaji na mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuongeza kazi katika utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 15 Agosti 2021 wakati alipofanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kukagua miradi ya maendeleo.
“Haiwezekani fedha zimeletwa hapa miezi mitano iliyopita hadi leo bado mpo kwenye hatua ya kuchimba mashimo ya nguzo ya jengo hili, uzembe huu haukubaliki kabisa, sio kwa wakati wangu” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ametoa miezi minne jengo hilo liwe limekamilika huku akimwagiza mkandarasi wa mradi huo, SUMA JKT kuongeza vibarua na mafundi na kutekeleza mradi huo usiku na mchana.
Mkuu wa Mkoa pia ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi kwa nini vifaa vya mradi huo havijanunuliwa viwandani moja kwa moja na badala yake vimenunuliwa katika maduka na kwa mawakala.
Mheshimiwa Hapi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kufuatilia matumizi ya shilingi milioni 37 zinazodaiwa zimetumika kununua nguzo, nyaya na vifaa vya umeme unaokuja kwenye mradi huo kuona uhalali wake.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Hapi ametoa siku saba kwa Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Bunda kuhakikisha mradi wa maji wa Iramba unaokarabatiwa uliotumia fedha zaidi ya shilingi milioni 473 unatoa maji kwa wananchi.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo baada ya kutokuridhishwa na maelezo ya RUWASA waliyoyatoa na hali halisi ya ukarabati wa mradi huo.
Mradi huo ulizinduliwa Januari 1978 na ukaharibika mwaka 2005 na serikali ikaleta fedha za kuukarabati shilingi milioni 500 tangu 2019 na mpaka sasa bado hautoi huduma ya maji kwa wananchi.
Katika siku ya kwanza ya ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Mheshimiwa Hapi ametembelea miradi miwili ya ujenzi wa barabara katika eneo la Iramba na Nyamswa, mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za halmashauri katika eneo la Kibara, mradi wa maji katika eneo la Iramba.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ameambatana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samweli Kiboye, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mheshimiwa Joshua Nassari na viongozi pamoja na watendaji wengine wa chama na serikali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa