Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo amepokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi wa matumizi ya fedha zinazotolewa na migodi kwa ajili ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika Mkoa wa Mara katika kipindi cha mwaka 2018/2019.
Akipokea taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa amevunja iliyokuwa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) ambayo iliundwa kinyume cha Sheria na miongozo kuhusiana na usimamizi wa fedha za umma ikisimamiwa na kamati iliyowashirikisha wawakilishi wa Mgodi wa North Mara na wananchi wa vijiji 11 vinavyouzunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
“CDC ilikuwa inatumika kama kichaka cha kupitisha miradi ya fedha za CSR ambazo kimsingi ni fedha za umma, kinyume cha sheria na taratibu za Serikali na bila kuwahusisha wataalamu wa Serikali waliopo katika Halmashauri na Wilaya ya Tarime” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amemuagiza Meneja Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa North Mara Bwana Apolinary Lyambiko kufanya mabadiliko ya Meneja Uhusiano wa Mgodi huo Bwana Gilbert Mworia ambaye alikuwa Katibu wa CDC ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazomkabili.
Mkuu wa Mkoa amemuagiza Kamanda wa Kipolisi wa Kanda Maalum ya Tarime- Rorya kufungua majalada maalum ya uchunguzi kwa viongozi wote wa CDC ikiwemo kuhoji walipata wapi mamlaka ya kuunda kamati ya kushughulikia fedha za umma kinyume cha sheria na taratibu za fedha za umma.
Aidha, Mheshimiwa Hapi amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuhakikisha migodi yote ya madini iliyopo katika Mkoa wa Mara ambayo haijafanya makubaliano na Halmashauri zinafanya makubaliano hayo ndani ya muda wa mwezi mmoja.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara ametoa maamuzi ya serikali kuhusiana na taarifa hiyo kuwa fedha zote za CSR kuwa ni fedha za umma na fedha hizo ni sehemu ya vyanzo vya mapato ya Halmashauri; miradi yote ya fedha za CSR itaibuliwa kuzingatia masuala muhimu ya uibuaji wa miradi ya serikali; uibuaji wa miradi ya CSR upite katika mfumo wa kawaida kuanzia ngazi za vijiji hadi Mkoa; na wataalamu wa Halmashauri washiriki katika kupanga hadi utekelezaji wa miradi hii.
Maamuzi mengine ni kuendelea kutumika kwa mfumo wa Force account katika miradi ya CSR; ushirikishwaji wa wananchi wanaozunguka mgodi katika utekelezaji wa miradi; ukokotoaji wa mapato ya migodi uwe shirikishi kwa wadau wote; manunuzi ya vifaa kuzingatia mahitaji ya mradi; fedha zote za mradi ziwekwe kwenye vijiji mradi unapotekelezwa; muda wa utekelezaji wa miradi kuzingatiwa.
Maamuzi mengine ni wajibu wa kusimamia miradi yote ya CSR ni wa Serikali kupitia Halmashauri na Migodi itapewa taarifa;miradi yote ya CSR kuwa ni mali ya Serikali; mafaili yote ya miradi hiyo yawepo katika eneo la mradi husika; na miradi hiyo iandaliwe upya katika mfumo wa kawaida wa Serikali na kuhusisha wataalamu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Uchunguzi Bwana Anselm Mwampoma ameeleza kuwa lengo la uchunguzi huo lilikuwa ni kubaini namna ambavyo rasilimali ya madini yaliyopo katika Mkoa wa Mara yanavyotumika katika miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mara.
Bwana Mwampoma ameeleza kuwa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ulikuwa umetoa jumla ya shilingi 5,750,000,000 katika kipindi hicho cha miaka mitano na kati ya fedha hizo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ilipokea shilingi bilioni 5.2 huku Halmashauri ya Mji wa Tarime ilipokea milioni 510.
Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 Mgodi ulikuwa umetenga kwenye bajeti Dola za Kimarekani 1.8 milioni kwa ajili ya CSR fedha ambazo bajeti yake ilipitishwa na CDC na kupita katika vikao mbalimbali hadi zilipozuiliwa kutumika na Serikali ya Mkoa wa Mara.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa migodi mingine ya inayofanyakazi zake katika Mkoa wa Mara ikiwemo MMG Gold Mine, Cata Mine, ZEM (T) LTD, pamoja na wachimbaji wadogo haikuwa imeanza kutoa fedha za CSR katika Halmashauri za Wilaya iliyopo kwa mujibu wa Sheria.
Kamati ya kuchunguza fedha za CSR katika Mkoa wa Mara iliundwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhandisi Gabriel Robert Luhumbi ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Wajumbe wa kamati ya uchunguzi walikuwa Bwana Anselm Mwampoma kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Marehemu Raphael Ndimbo, Usalama wa Taifa, Bwana Ramadhani S. Nkunya kutoka ofisi za TAKUKURU (M), Byalugaba C. Byalugaba kutoka Ofisi ya Madini (M) na Bwana Samson William kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Mapokezi ya taarifa hiyo yamehudhuriwa na Wajumbe wa Kamati ya Siasa (CCM) ya Mkoa wa Mara Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Baadhi ya Taasisi, wenyeviti wa halmashauri, Kamati ya Usalama ya Mkoa, viongozi wa dini, wamiliki wa migodi na wachimbaji wadogo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa