Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 10 Novemba 2021 amepiga marufuku kwa Halmashauri kununua vifaa vya ujenzi kama vile mbao, nondo, mabati na saruji kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kununuliwa rejareja kwa wafanyabiashara badala ya kuagiza kwa pamoja viwandani.
Mheshimiwa Hapi amepiga marufuku hiyo alipokuwa anaendelea na ziara ya siku tatu kukagua miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule za Sekondari na Shule Shikizi za Msingi katika Wilaya za Rorya, Tarime na Serengeti.
“Mwongozo wa Serikali na Mkoa ni kuwa vifaa vyote vinunuliwe kwa ujumla kutoka viwandani ili fedha hizi ziweze kutosheleza mahitaji katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, atakayepindisha tutashughulika nae kabla hatujashughulikiwa sisi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amewataka Wakurugenzi na Watendaji wa Halmashauri kufuata maelekezo yote ya Serikali yaliyotolewa pamoja na fedha hizo na kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa hadi kufikia tarehe 1 Desemba 2021.
Mheshimiwa Hapi ameikemea Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa kuwatumia baadhi ya wakandarasi katika kujenga vyumba vya madarasa ambao wanatuhumiwa katika miradi mingine ambapo suala hilo lipo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na uchunguzi wake unaendelea.
“Haiwezekani kazi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa mnawapa wazabuni ambao baadhi yao wanatuhumiwa kupewa zabuni katika miradi iliyotelekezwa vibaya katika Halmashauri hii na uchunguzi wake upo TAKUKURU unaendelea” alisema Mheshimiwa Hapi.
Wazabuni waliopewa kazi ya kujenga vyumba hivyo ni pamoja na Dapol Construction (08), Juma Kenan (04), Afiki Mara Investment (05) Jura Tanzania Limited (60) huku mafundi wa kawaida wakipatiwa vyumba 10 na kubakia na vyumba 29 ambavyo bado mafundi wanatafutwa.
Mkuu wa Mkoa amezitaka Halmashauri katumia miradi hii kujenga ofisi za walimu hususan katika shule ambazo zimepatiwa madarasa mengi ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Mheshimiwa Hapi akiwa katika Wilaya ya Tarime alikagua ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari ya Mogabiri, ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi katika Shule Shikizi ya Msingi ya Kedere na ujenzi wa vyumba vya madarasa vinne katika Shule ya Sekondari ya Ingwe.
Katika Wilaya ya Serengeti, Mkuu wa Mkoa alikagua ujenzi wa vyumba sita vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Mapinduzi Day na vyumba vya madarasa manne katika Shule ya Sekondari ya Serengeti.
Katika vyumba vya madarasa vinavyojengwa kutokana na fedha za Mpango wa Maendeleo na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, Halmashauri ya Mji wa Tarime imepewa vyumba vya madarasa 32, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime imepewa vyumba vya madarasa 116 wakati Hamashauri ya Wilaya ya Serengeti imepatiwa vyumba vya madarasa 102.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samwel Kiboye, Wakuu wa Wilaya za Tarime na Serengeti na baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usalama za Wilaya, madiwani na watumishi wa halmashauri.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji ameeleza kuwa kwa sasa kuna miradi ya vmadarasa katika shule tatu ambayo kazi ya kunyayua ukuta imeshaanza lakini mingine ipo katika hatua ya msingi.
“Hata hivyo miradi ya ujenzi imepata changamoto baada ya pampu ya maji kuungua katika mradi wa maji wa Manchira na hivyo Mji wa Mugumu kukosa maji ya uhakika na hivyo kukwamisha shughuli za ujenzi kuendelea vizuri” alisema Mheshimiwa Mashinji.
Hata hivyo ameeleza kuwa tayari kifaa kilichoungua kilikuwa kimepatikana na mafundi walikuwa wanaendelea kurekebisha pampu hiyo na maji yalikuwa yanategemea kurejea katika hali ya kawaida muda sio mrefu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa