Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 25 Julai, 2022 amewaongoza wananchi wa Mkoa wa Mara kufanya usafi, kuomba dua na kutoa heshima ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya mashujaa.
Kumbukumbu hiyo ilianza saa 12.00 asubuhi kwa kufanya usafi katika Soko la Saa Nane lililopo katika Manispaa ya Musoma ambapo Mheshimiwa Hapi aliwahamasisha wananchi kufanya usafi katika maeneo yao ili kuweza kudhibiti magonjwa yanayotokana na uchafu.
“Magonjwa yanayotokana na uchafu ni mengi na yanatumia gharama kubwa kuyatibu yasipodhibitiwa katika kufanya usafi vizuri katika maeneo tunayoishi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha, akiwa katika eneo hilo Mheshimiwa Hapi amezindua rasmi ghuba la kuwekea uchafu na kuiagiza Manispaa ya Musoma kuondoa dampo lisilo rasmi kwenye makazi ya watu katika Soko la Saa Nane na badala yake takataka zitupwe katika ghuba hilo.
Mheshimiwa Hapi pia alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi waliojitokeza kufanya usafi kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 ambayo itafanyika hapa nchini tarehe 23 Agosti, 2022.
“Sensa hii itaiwezesha Serikali kujua idadi ya watu, mahitaji yao ya msingi na nini kifanyike katika kuwaletea maendeleo wananchi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Baada ya usafi, msafara ukaelekea Parokia ya Kanisa Katoliki Rwamlimi ambapo kuna mnara wa kumbukumbu ya ndege ya kivita iliyoanguka katika eneo hilo wakati wa vita vya Kagera.
Katika eneo hilo, kulikuwa na dua kutoka kwa viongozi wa dini, gwaride la heshima pamoja na salamu kutoka kwa viongozi mbalimbali.
Akizungumza katika eneo hilo, Mheshimiwa Hapi amewataka wananchi kuwaenzi mashujaa wa Taifa letu kwa kutenda mazuri waliyokuwa wanayapigania na kudumisha umoja, amani na mshikamano wa Taifa.
Kumbukumbu ya Mashujaa kitaifa ilifanyika Kitaifa katika Mkoa wa Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa