Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 29 Januari 2022 ameongoza matembezi ya hamasa yaliyowahusisha watumishi wa umma na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Matembezi hayo ni sehemu ya maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan atakayoifanya katika Mkoa wa Mara hivi karibuni.
Akizungumza baada ya matembezi hayo Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa lengo la matembezi hayo ni maandalizi ya kumpokea Mheshimiwa Rais atakapofanya ziara katika Mkoa wa Mara.
“Tunategemea Mheshimiwa Rais atashiriki matembezi katika eneo hili ambalo tumepita leo, hivyo kila mtu ameona mapungufu au changamoto kwenye eneo kulingana na majukumu yake, tukazifanyie kazi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha Mheshimiwa Hapi amezitaka TARURA, TANROADS, Manispaa ya Musoma na taasisi zote za umma zilizopo mkoani Mara kuhakikisha kuwa eneo hilo linapitika vizuri, safi lipo tayari kutumika katika matembezi hayo.
Matembezi ya hamasa yalianzia katika Ikulu Ndogo ya Mkoa wa Mara kupitia barabara za Boma, Mkendo, Uhuru hadi katika Ofisi za Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara umbali wa takriban kilomita 3.2.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atafanya ziara ya kikazi mwanzoni mwa mwezi wa Februari katika Mkoa wa Mara ambapo pamoja na mambo mengine atashiriki matembezi kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 45 ya CCM ambayo kitaifa yatafanyika katika Mkoa wa Mara.
Matembezi hayo yalihudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Katibu wa Mkoa wa CCM, Mkuu wa Wilaya ya Musoma pamoja watumishi na viongozi wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa