Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 5 Agosti 2021 ameongoza kikao cha maandalizi ya Siku ya Mara inayotarajia kufanyika tarehe 15 Septemba 2021 katika Wilaya ya Tarime.
Akizungumza katika kikao hicho Mheshimiwa Hapi amewataka wadau wa utalii na mazingira kuchangia maandalizi ya siku hiyo ili iweze kufana na kuwahamasisha wadau waweze kushiriki.
“Niwaombe wadau wote waweze kushiriki katika kuchangia maandalizi ya Siku ya Mara sio tu kwa fedha lakini hata kwa mawazo ili maadhimisho haya yaweze kuboreshwa na kuwa mazuri zaidi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameiagiza kamati ya maandalizi ya Siku ya Mara kuitangaza siku hiyo kitaifa na kimataifa ili kuimarisha jina la Mkoa wa Mara kwa wadau wake wa ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Hapi amewataka Wakuu wa Wilaya kufufua siku za usafi na vikundi vya kufanya mazoezi katika wilaya zao ili kuimarisha afya za wananchi wa Mkoa wa Mara.
Aidha katika kutengeneza jina la Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Hapi amesimamisha mashindano yote ya mbio yanayoitwa Serengeti katika Mkoa wa Mara hadi hapo Mkoa utakapopata mbio ambazo zitakazoutambulisha mkoa kitaifa na kimataifa.
Maadhimisho ya Siku ya Mara ni ya kimataifa yenye lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira yanayouzunguka Mto Mara ambao unaanzia katika milima ya Mai nchini Kenya na kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria katika Mkoa wa Mara.
Maadhimisho ya Siku ya Mara yanafanyika kila mwaka katika nchi za Kenya na Tanzania yakihusisha wadau mbalimbali hususa wadau wa utalii, maji na mazingira.
Wakati huo huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela ameeleza kuwa Mkoa wa Mara pia unaandaa Maonyesho ya Teknolojia ya Madini na Wajasiriamali yatakayofanyika Oktoba 2021 katika eneo la Bweri nyuma ya stendi kuu ya mabasi.
Bwana Msovela ameeleza kuwa maonyesho hayo yatahusisha wadau wa madini na ujasiriamali kutoka katika Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mara, Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Kagera na Geita.
“Mpaka sasa tumeshapata eneo la ekari 10.3 kwa ajili ya maonyesho hayo na lipo katika eneo la Bweri katika Manispaa ya Musoma” alisema Bwana Msovela.
Ameeleza kuwa awali kulikuwa na mpango wa kuandaa maonyesho ya madini na baadaye likaja wazo la kuunganisha na wajasiriamali wadogo ili kuyapa nguvu zaidi maonyesho hayo.
Kikao kingine cha maandalizi ya shughuli hizi kinategemewa kufanyika tena tarehe 17 Agosti, 2021 katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa