Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amekitaka Chuo cha Uganga Musoma (Musoma COTC) kujiimarisha kwa kuanza kukarabati na kuongeza miundombinu kwa kutumia mapato ya ndani.
Mheshimiwa Hapi ametoa maagizo hayo leo tarehe 2 Agosti 2021 wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Musoma.
“Kwa kutumia mapato ya ndani mnauwezo wa kuanza kukarabati chuo hiki hata jengo moja moja na kuanza kujenga majengo mengine pia” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha amekitaka kupanuka kwa kutafuta eneo kubwa ili kiweze kukua zaidi na kuchukua wanachuo wengi zaidi kwa manufaa ya taifa.
Mheshimiwa Hapi amesema kuwa Chuo hicho kinapaswa kuchangamkia fursa ya mpango wa kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia ambapo kikikamilika kinatarajiwa kuwa na kampasi yake katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
“Hapo zitatolewa kozi za fani mbalimbali za afya ya binadamu, mkikitumia vizuri mtapata wahadhiri, sehemu ya wanachuo wenu kufanya mazoezi ya vitendo na wataalamu wengineo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amekipongeza Chuo hicho kwa kufundisha vizuri wanachuo pamoja na upungufu wa watumishi uliopo katika Chuo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Ibrahim A. Bakari ameeleza kuwa Chuo hicho kwa sasa kina upungufu mkubwa wa wafanyakazi.
“Kwa sasa Chuo kina wafanyakazi 12 na kina upungufu wa wafanyakazi 37 na kati ya wafanyakazi waliopo wakufunzi ni saba tu ikilinganishwa na mahitaji ya wakufunzi 25 kulingana na idadi ya wanafunzi” alisema Dkt. Bakari.
Dkt. Bakari ameeleza kuwa ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa wafanyakazi wamekuwa wakiwatumia zaidi wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara pamoja na vituo vingine vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika Mkoa wa Mara.
Aidha ameeleza kuwa Chuo hicho kimefanikiwa kuongeza makusanyo baada ya jitihada za kuongeza wanafunzi lakini kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya upungufu na uchakavu wa miundombinu.
Mheshimiwa Hapi akiwa chuoni hapo pamoja na ujumbe alioambatana nao alikagua mazingira, akazungumza na wanachuo na watumishi wa Chuo hicho.
Chuo cha Uganga Musoma kilianzishwa miaka ya 1970 na miundombinu yake mingi ilijengwa wakati huo na kinatoa Stashahada za Uuguzi na Udaktari pamoja na Astashahada ya Udaktari.
Mheshimiwa Hapi aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Alfany Haule, watumishi wa Manispaa ya Musoma.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa hapi alitembelea Kiwanda cha Samaki cha Alpha, Shule ya Sekondari ya Mara, Shule ya Msingi Kigera A, Kituo cha Afya Mshikamano na mradi wa ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa