Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo amehudhuria kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na kukemea mivutano inayoendelea katika halmashauri hiyo baina ya madiwani.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa amepata taarifa za malumbano ya viongozi na wananchi wa wilaya hiyo tangu wilaya ilipoanza mpaka sasa na matokeo ya malumbano hayo ni kuchelewesha miradi ya maendeleo ya wananchi.
“Mheshimiwa Rais analeta fedha hapa zifanye maendeleo, lakini badala yake fedha zinakuja na hazitumiki kwa sababu mnavutana kila mtu anataka mradi ujengwe katika eneo lake, huku mkiendelea kuwaumiza wananchi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Halmashauri hiyo imepokea fedha kuanzia tarehe 25 Februari, 2022 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Labour, lakini mpaka sasa mradi huo umesimama kwa sababu madiwani wanabishana sehemu ya kujenga kituo hicho.
“Sasa, ninatoa siku saba ujenzi wa Kituo cha Afya Labour uwe umeanza na ninahitaji taarifa ya utekelezaji wa mradi huu”aliagiza Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa anafahamu kikao cha baadhi ya madiwani wa Halmashauri hiyo kilichokaa Sirari katika Wilaya ya Tarime kupanga njama ya kumuondoa madarakani Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mheshimiwa Ng’ong’a Gerald Samweli na viongozi wengine katika wilaya hiyo na kuwataka madiwani hao kuacha mara moja.
Aidha, Mheshimiwa Hapi amewaonya wanamara wanaochochea malumbano yasiyo na tija katika Mkoa wa Mara na kukwamisha miradi ya maendeleo ya wananchi kuacha tabia hiyo.
Mheshimiwa Hapi amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha madeni yote ambayo Halmashauri inadai yanalipwa ili kuiwezesha Halmashauri hiyo kulipa madeni yake ikiwemo madeni ya posho za vikao vya madiwani.
Mheshimiwa Hapi amewaonya madiwani kuacha malumbano mara moja na wakiendelea na malumbano hayo Mkoa utamshauri Mheshimiwa Rais kuvunja Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Makongorosi na Urio katika Kata ya Labour, Mheshimiwa Hapi amewataka wananchi wa Kata hiyo kushikama ili kufanikisha maendeleo ya Kata hiyo.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Bwana Langaeli Akiyoo ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Rory ana kuwataka madiwani wasimamie utekelezaji wa miradi.
“Ninawaomba msimamie utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi waliowachagua” alisema Bwana Akyoo.
Bwana Akyoo amewakubusha madiwani kuwa wapo katika Baraza hilo kwa sababu wananchi na vyama vyao viliwaamini watawaletea maendeleo katika eneo hilo, wasiipoteze imani hiyo.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mheshimiwa Juma Chikoka ameeleza kuwa umoja na mshikamano ni muhimu sana wakati huu ambapo Serikali inaleta fedha za kuijenga Rorya.
Akizungumza wakati wa kikao cha Baraza hilo, Mheshimiwa Chikoka ameemeza kuwa kwa sasa kipaumbele kikubwa kwa Wilaya ya Rorya ni kuinua mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo ili yaweze kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi.
“Mapato yakiimarika Halmashauri itakuwa na uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo na kutoa mikopo kwa makundi mbalimbali ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa mujibu wa Sheria” alisema Mheshimiwa Chikoka.
Mheshimiwa Chikoka ameeleza kuwa kwa sasa Halmashauri inampango wa kuanzisha stendi mpya ya mabasi katika eneo la Mika na shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo katika bajeti yam waka ujao wa fedha.
Aidha, Mheshimiwa Chikoka ameeleza kuwa Halmashauri pia inaongeza nguvu za uwekezaji katika mazao ya biashara ya pamba, alizeti na kahawa na viongozi wa Wilaya ya Rorya watakuwa na mashamba ya mfano ya mazao haya.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa