Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ametembelea Wilaya ya Rorya na Tarime kukagua maandalizi ya ujenzi wa miradi ya madarasa na vituo vya afya vilivyotengewa fedha na serikali.
Mheshimiwa Hapi ametembelea maeneo hayo leo tarehe 16 Oktoba 2021 na kutoa maelekezo kwa viongozi kuhusiana na maandalizi hayo.
“Lengo la ziara hiii ni kuangalia maeneo ambapo miradi hii itajengwa pamoja na kukagua maandalizi ya kuanza kwa miradi hii mara baada ya fedha kuruhusiwa kuanza kutumika.
Mheshimiwa Hapi alitembelea mradi wa upanuzi wa zahanati kuwa Kituo cha Afya Nyamagaro na ujenzi wa Madarasa katika Shule ya Sekondari ya Nyamtinga katika Wilaya ya Rorya.
Aidha akiwa katika Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Hapi alitembelea mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya katika eneo la Kitenga katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na mradi wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari ya Nkende katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Akizungumza na wakati akitembelea miradi hiyo Mheshimiwa Hapi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea na maandalizi ya ujenzi huo pamoja na kuunda kamati za ujenzi huo mapema iwezekanavyo.
Aidha Mheshimiwa Hapi amevielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia miradi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua watu wote watakaohusika na ubadhilifu wa aina yoyote ile katika miradi hiyo.
Mheshimiwa Hapi amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha barabara ya kuingia katika Shule ya Sekondari Mtinge inapitika muda wote.
Aidha amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha maeneo ambayo miradi hii inaenda kujenga hayana migorogo na wananchi.
“Serikali haina fedha za kuanza kulipa watu fidia, kama maeneo yaliyoainishwa katika miradi hii yana mgogoro, leteni mapendekezo ya kupeleka miradi hiyo maeneo mengine haraka iwezekanavyo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amewataka watendaji wote watakaohusika katika utekelezaji wa miradi hiyo kutimiza wajibu wao kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma za kijamii zinazokusudiwa kutoaka na miradi hiyo.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa pia alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi wa eneo la Nyamagaro katika Wilaya ya Rorya na maeneo ya Kitenga na Nkende katika Wilaya ya Tarime.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliambatana na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Mwakilishi wa Afisa Elimu wa Mkoa, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri na watendaji wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa