Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameitaka Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma itumie uwezo iliyonayo ili kujiongezea mapato yanayotokana na kazi za ufundi wa kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Mheshimiwa Hapi ametoa kauli hiyo leo tarehe 23 Novemba 2021 wakati alipokuwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa, utengenezaji wa matofali pamoja na utengenezaji wa viti na meza kwa ajili ya vyumba vya madarasa katika Wilaya ya Musoma.
“Kwa mashine, wataalamu na nguvu kazi iliyopo hapa, mnauwezo wa kutengeneza viti, meza, vitanda, milango, madirisha, magari na kadhalika mkaviuza kwa bei ya soko ili kuongeza mapato ya Shule na utaalamu wa vitendo kwa wanafunzi na walimu pia” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza viti na meza vinavyotengenezwa vinaubora na gharama yake ni nafuu ikilinganishwa na ubora uliopo mitaani na kuwataka waongeze uzalishaji ili kiwe kituo cha kununua mahitaji kwa taasisi na watu binafsi.
Aidha Mheshimiwa Hapi amewataka wanafunzi wanaosoma masomo ya ufundi kufanyakazi kwa bidii ili waweze kupata elimu, ujuzi na uzoefu kwa vitendo katika kuunda na kutengeneza vitu mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mlezi wa Shule hiyo, ameipongeza shule hiyo kwa kutekeleza kwa haraka maagizo aliyoyatoa awali kuhusu kufufua mashine zilizopo katika shule hiyo ili kuweza kupata kazi mbalimbali.
Aidha ameipongeza Shule hiyo kwa kupiga hatua katika mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuwa mfano katika Manispaa ya Musoma ambapo ujenzi wa boma umeshakamilika na wanatarajia kuanza kuezeka.
Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma Mwalimu Mohamed Kajeri ameeleza kuwa kwa sasa Shule hiyo imepokea oda ya kutengeneza viti na meza kutoka katika Halmashauri tano za Mkoa wa Mara.
Mwalimu Kajeri ameeleza kuwa kutokana na mpangokazi wao walivyojipanga, wanatarajia kukamilisha kutengeneza viti na meza hizo ndani ya wiki mbili na tayari vifaa vilikuwa vimeshanunuliwa msafara ulishuhudia mbao na vyuma vikiwa vinashushwa shuleni hapo.
Aidha Mwalimu Kajeri Amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwapa wazo la kuanza kujitegemea bidhaa mbalimbali kwa kutumia wataalamu na vifaa vilivyopo na kwa sasa wanapata wateja hususan kutoka katika taasisi za umma.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa pia ametembelea mradi wa ujenzi wa madarasa matatu na ofisi moja katika Shule ya Sekondari Mugango, mradi wa kufyatua matofari wa Kikosi cha Jeshi Makoko katika eneo la Bukima katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Mheshimiwa Hapi pia ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Nyasho, mradi wa ujenzi wa vyumba viwili na ofisi moja na karakana ya kutengeneza bidhaa mbalimbali katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma katika Manispaa ya Musoma.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, viongozi wa Chama cha Mapinduzi, Wakurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Manispaa ya Musoma, wakuu wa idara na watendaji wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa